Iran inatoa viza ya siku 30 uwanja wa ndege kwa nchi 180
(last modified Sun, 14 Feb 2016 07:06:57 GMT )
Feb 14, 2016 07:06 UTC
  • Iran inatoa viza ya siku 30 uwanja wa ndege kwa nchi 180

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vituo vya uwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje katika mikoa na viwanja vya ndege vinatoa viza ya siku 30 kwa raia wa nchi 180 duniani.

Sayyid Abbas Araqchi, ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayehusika na masuala ya kisheria na ya kimataifa ameyasema hayo katika kikao cha pamoja na wakuu wa mikoa, mameya wa miji, pamoja na rais na wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara wa Iran huko mkoani Esfahan katikati mwa Iran. Akiashiria mchango muhimu wa sekta ya utalii katika ustawi wa kiuchumi wa mataifa Araqchi amesema makubaliano ya nyuklia (JCPOA) ni fursa mwafaka ya kuondoa kasoro na mapungufu ya kiuchumi na kuiletea Iran ustawi na maendeleo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa wizara hiyo imeliweka suala la diplomasia ya kiuchumi kwenye ajenda za kufanyiwa kazi na balozi pamoja na vituo vya uwaklishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi mbalimbali.

Araqchi amesisitiza kuwa kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia kumefungua ukurasa mpya wa fursa kwa Iran katika uga wa kimataifa ambazo inapasa kunufaika nazo.

Akiashiria utafiti wa hivi karibuni wa kituo cha utafiti cha Marekani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kwa mujibu wa uchunguzi huo endapo Iran itachukua hatua sahihi kiuchumi, ifikapo mwaka 2025 itakuwa moja ya nchi tajiri zaidi duniani.../

Tags