Kiongozi Muadhamu atilia mkazo wajibu wa kupambana na wavamizi
(last modified Thu, 09 Jan 2025 03:21:16 GMT )
Jan 09, 2025 03:21 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atilia mkazo wajibu wa kupambana na wavamizi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesisitizia wajibu wa kupambana na uvamizi wa Marekani nchini Iraq. Ametoa mwito huo wakati alipoonana na Waziri Mkuu wa Iraq na ujumbe alioongozana nao waliokwenda kumtembelea ofisini kwake hapa Tehran jana Jumatano.

Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza kuwa, katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Jumatano jioni, Imam Khamenei amemwambia Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia'a al-Sudani kwamba kuwepo majeshi ya Marekani nchini Iraq ni kinyume cha sheria na ni dhidi ya maslahi ya wananchi na serikali ya Iraq na kusisitiza kuwa, ushahidi unaonesha kwamba Wamarekani wanafanya njama za kuimarisha uwepo wao wa kivamizi katika ardhi ya Iraq, suala ambalo inabidi kukabiliana nalo kwa nguvu zote.

Imam Khamenei aidha ameashiria matukio ya eneo hili hususan hali ya Syria na kusisitiza kuwa, nafasi ya serikali za kigeni katika masuala hayo iko wazi kabisa.

Vilevile Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uhusiano mzuri uliopo kati ya serikali na wananchi wa Iraq, ameutaja umoja na mshikamano baina ya dini na makabila mbalimbali ya Iraq kuwa ni jambo la lazima na muhimu sana na kumsisitizia Waziri Mkuu wa Iraq akimwambia, kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al-Hashd al-Shaabi ni moja ya nguzo muhimu katika muundo wa kiusalama na kijamii wa Iraq, inabidi nguzo hiyo ilindwe na kuimarishwa zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma.

Vilevile amepongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya Iraq katika kuleta ustawi na kudumisha usalama nchini Iraq na kusema: "Kadiri Iraq inavyostawi na kuwa salama zaidi ndivyo inavyokuwa bora zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia'a Al-Sudani ameeleza kuridhishwa kwake na mazungumzo yake aliyofanya na viongozi mbalimbali wa Iran hapa Tehran na kueleza matumaini yake kuwa mazungumzo na mapatano hayo yatapanua zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.