Iran yapongeza kuchaguliwa rais mpya nchini Lebanon, yasisitiza kustawishwa uhusiano
Jan 10, 2025 10:30 UTC
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempongeza Rais mpya wa Lebanon, Serikali na wananchi wake pamoja na mirengo na vyama vyote husika katika uga wa kisiasa wa nchi hiyo kwa kuchaguliwa rais mpya.
Katika taarifa aliyotoa Alkhamisi usiku, Ismail Beqaei alisema, kuchaguliwa Jenerali Joseph Aoun, ambako kumetokana na mwafaka na makubaliano baina ya akthari ya makundi na vyama vya siasa, ni mafanikio kwa Lebanon yote, na akaeleza matumaini yake kwamba kuchaguliwa kwa Aoun kutaimarisha umoja na mshikamano ndani ya Lebanon na kurahisisha njia ya maendeleo na ustawi wa nchi hiyo na kufanikiwa kuzishinda changamoto na matatizo yaliyo mbele yake, yakiwemo ya kiuchumi, kukarabati uharibifu uliosababishwa na uchokozi wa kinyama uliofanywa na utawala wa Kizayuni, na kulinda mamlaka ya kitaifa na ukamilifu wa ardhi yote ya Lebanon dhidi ya vitisho na uchu wa utawala ghasibu wa Kizayuni.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria pia uhusiano wa kihistoria kati ya nchi mbili na kusisitiza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kustawisha uhusiano na serikali ya Lebanon katika nyuga zote sambamba na kumtakia mafanikio mema rais mpya wa nchi hiyo.
Jenerali Joseph Aoun alichaguliwa kuwa Rais wa Lebanon jana Alkhamisi Januari 9, 2025 kwa kura 99 za 'ndiyo' katika duru ya pili ya kura zilizopigwa na wabunge. Hii ni mara ya tano katika historia ya Lebanon kwa kamanda wa jeshi kushika wadhifa wa urais.../
Tags