Iran yataka OIC iitishe mkutano wa dharura kuijadili Gaza
(last modified Sun, 09 Feb 2025 07:11:47 GMT )
Feb 09, 2025 07:11 UTC
  • Iran yataka OIC iitishe mkutano wa dharura kuijadili Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amekosoa vikali mpango wa pamoja wa Marekani na Israel wa kuwahamisha raia wa Gaza, na maangamizi ya kizazi katika eneo hilo lililozingirwa.

Katika mazungumzo kwa njia ya simu jana usiku na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Hussein Ibrahim Taha, Araghchi amesema mataifa yote ya Kiislamu lazima yachukue msimamo mmoja kuzuia njama hiyo ya kutaka kuinyakua na kuitwaa Gaza.

Waziri Araghchi ametoa wito wa kufanyika mkutano wa dharura wa jumuiya hiyo kubwa ya Waislamu duniani, ili kuchukua hatua madhubuti za kutetea haki za Wapalestina. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameashiria wajibu mkubwa wa mataifa ya Kiislamu kuunga mkono haki za Wapalestina wanaodhulumiwa, hususan haki yao ya kujitawala.

"Mpango wa kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza sio tu uhalifu mkubwa unaoshabihiana na 'mauaji ya halaiki,' lakini pia una madhara ya hatari kwa utulivu na usalama wa eneo hilo na dunia," amesisitiza Araghchi.

Araghchi katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty

Jana jioni pia, Araghchi katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty alitoa mwito huo huo wa kuitishwa mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuhusu Gaza.

Mpango huo haramu wa Trump kuhusiana na Gaza umepata upinzani mkali kutoka kwa nchi mbalimbali duniani.