Wizara ya Mambo ya Nje: Iran haikubali mazungumzo chini ya mashinikizo
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haikubali mazungumzo chini ya mashinikizo, na kutangaza kuwa: Katika kuendeleza utendaji wake wa kisheria, Iran, daima inaunga mkono suuala la kupatiwa ufumbuzi masuala mbalimbali kwa njia za kidiplomasia ikiwa ni pamoja na suala la nyuklia.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambayo imetolewa kujibu Notisi ya Usalama wa Taifa ya Rais Donald Trump wa Marekani na kueleza kuwa: Rais wa Marekani Februari 4 mwaka huu alisaini Notisi ya Usalama wa Taifa na kuamuru kuhuishwa sera zilizofeli za nchi hiyo kwa jina la "mashinikizo ya kiwango cha juu' dhidi ya taifa la Iran.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa: Serikali ya Marekani inadai kufufua mashinikizo ya juu lakini hakuna wakati mashinikizo hayo ya kiwango cha juu yalisitishwa ili leo hii yaanzishwe tena. Serikali iliyotangulia ya Marekani hakusimamisha hata kikwazo kimoja dhidi ya Iran, na kama ilivyokiri yenyewe, imezidisha mamia ya vikwazo kwenye vikwazo vilivyotangulia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu imedhihirisha kuwa inajibu "mashinikizo ya kiwango cha juu" kwa "muqawama wa kiwango cha hali ya juu" na inaamini kwa dhati kwamba hakuna nchi inayopasa kukabiliwa na mashinikizo kinyume cha sheria na vikwazo haramu.
Ikumbukwe kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzu ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amekutaja kufanya mazungumzo na Wamarekani katika mazingira ya sasa kuwa si jambo la werevu, mantiki, wala heshima kutokana na tajiriba ya historia na rekodi ya utendaji ya serikali ya Marekani.
