Rais wa Iran: Waislamu wanapaswa kuwa na mchango athirifu katika kukabiliana na watendajinai duniani
(last modified Tue, 01 Apr 2025 15:18:22 GMT )
Apr 01, 2025 15:18 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian
    Rais Masoud Pezeshkian

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na viongozi wa nchi mbalimbali, akiwapongeza kwa mnasaba wa kusherehekea sikukuu ya Idul-Fitr. Amesisitiza ulazima wa kuimarishwa zaidi umoja na uhusiano wa kindugu baina ya nchi za Waislamu na ulazima wa kuzima njama za maadui.

Akizungumza kwa simu na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria, Rais Masoud Pezeshkian ametoa pongezi kwa taifa na serikali ya nchi hiyo kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul-Fitr na kuwaombea Mungu atakabali dua na maombi yao na kuwapa izza na fahari. Amesema: "Watu wa Algeria na Waislamu wote dunia kwa ujumla, wanapaswa kuwa na mchango athirifu katika kukabiliana na maadui watendajinai dunia na kuwahami na kuwatetea watu wanaodhulumiwa, hususan watu wa Ukanda wa Gaza, kwa kuzidisha umoja, mshikamano na undugu wao."

Kwa upande wake, Rais wa Algeria pia ametoa salamu za Idul-Fitr kwa serikali na wananchi wa Iran, akieleza matumaini yake kuwa uhusiano wa Algeria na Iran utapanuka zaidi kwa kuzingatia mambo yanayozikutanisha pamoja pande mbili, kuheshimiana na kunufaishana.

Marais Pezeshkian na Tebboune

Rais Pezeshkian pia amefanya mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' Al Sudani , ambapo amewapongeza wananchi na serikali ya Iraq kwa kuadhimisha sikukuu ya Idul-Fitr na kuwatakia mafanikio katika maombi na ibada zao. Amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapenda kupanua uhusiano katika nyuga mbalimbali na rafiki, ndugu na jirani yake wa muda mrefu, Iraq."

Waziri Mkuu wa Iraq pia amesema: Kuimarishwa undugu na uhusiano wa kirafiki kati ya Iran na Iraq ni jambo la dharura kwa nchi hizo mbili katika eneo nyeti la Asia Magharibi. Mohammad Shia al-Sudani amesema, umoja na misimamo ya nchi hizo mbili inapaswa kuimarishwa zaidi dhidi ya watu wenye nia mbaya kwa mataifa hayo mawili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu pia amewasiliana na marais wa nchi za Tajikistan na Uzbekistan akiwapongeza wao na mataifa yao kwa mnasaba wa kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea sikukuu ya Idul Fitr. Vilevile ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano na uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni baina ya Iran na nchi hizo.