Iran yapiga shabaha 150 za Israel katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3
(last modified Sat, 14 Jun 2025 07:13:46 GMT )
Jun 14, 2025 07:13 UTC
  • Iran yapiga shabaha 150 za Israel katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3

Afisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Iran amesema kwa akali shabaha 150 zimepigwa wakati wa operesheni ya kulipiza kisasi ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya utawala haramu wa Israel, ikiwa ni pamoja na kambi kadhaa za kimkakati za kijeshi za utawala huo pandikizi.

Akizungumza mapema leo Jumamosi, Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, Mshauri Mkuu wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), amesema Operesheni ya Ahadi ya Kweli III imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na kikosi cha anga cha IRGC.

"Malengo haya yalifikiwa kwa mafanikio katika awamu nyingi," Brigedia Jenerali Vahidi, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika utawala wa marehemu Ebrahim Raeisi, amesema.

Afisa huyo aliorodhesha baadhi ya shabaha zilizopigwa kuwa ni pamoja na kambi za ndege za kijeshi za Nevatim na Ovda, zilizoko katika maeneo ya kaskazini-kati na kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Tel Aviv unateketea kwa makombora ya Iran

Brigedia Jenerali Vahidi ameongeza kuwa, operesheni hiyo imetoa "pigo kubwa" kwa utawala wa Kizayuni, na kudhihirisha "maonyesho makubwa ya nguvu," na kusisitiza kwamba hujuma hizo zinaweza kufanyika tena iwapo italazimu.

Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeanza kutekeleza wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel, ili kulipiza kisasi kufuatia hujuma za utawala huo wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran.

Awamu ya tatu ya operesheni ya kijeshi ya kulipiza kisasi ya Iran - Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3 - ilianza mwendo wa saa saba na nusu usiku wa kuamkia leo kwa saa za hapa Iran, baada ya awamu mbili zenye mafanikio, ambapo maeneo mengi ya kimkakati ya Israel yalilengwa.

Iran yaipa kipigo Israel

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilisema vitengo vya makombora na ndege zisizo na rubani vililenga kambi za jeshi la Israel ambazo zilitumiwa kuanzisha mashambulio dhidi ya Iran, pamoja na utengenezaji wa silaha za kiviwanda na maeneo mengine ya kijeshi ndani ya Israel.