IRGC: Nguvu ya kijeshi ya Iran imesambaratisha mikakati ya Israel
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema kwamba uwezo wa Iran wa kijeshi hasa wa kushambulia na kujilinda ulifanikiwa kuvuruga kabisa mikakati ya utawala wa Israel wakati wa siku 12 za mashambulizi ya kimabavu.
Msemaji wa IRGC, Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini alitangaza Jumapili kwamba, “Utawala wa Kizayuni ulishangazwa na vita vilivyodumu kwa siku 12. Kama mashambulizi ya makombora ya majeshi ya Iran yangeendelea, hakungebaki kitu kuhusu utawala huo leo."
Jenerali Naeini alipuuzilia mbali kauli zinazotolewa na Waziri wa Mambo ya Kijeshi wa Israel dhidi ya Iran, akizitaja kuwa mbinu za vita vya kisaikolojia. Hata hivyo, amesisitiza kuwa majeshi ya Iran yanaendelea kujiimarisha zaidi.
Naeini alieleza kuwa nguvu laini ya Iran, inayotegemea mwongozo wa busara wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, imani za kidini za watu na mshikamano wa kitaifa, imefanikiwa kuzima njama za maadui.
Mnamo Juni 13, Israel ilianzisha vita bila sababu dhidi ya Iran, ikiwalenga makamanda wa ngazi ya juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida.
Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani iliingia vitani kwa kushambulia kwa mabomu maeneo matatu ya nyuklia ya Iran, ikiwa ni ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Katika kujibu, majeshi ya Iran yalishambulia vituo nyeti katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu pamoja na kituo cha kijeshi cha al-Udeid kilichopo Qatar, ambacho ni kituo kikubwa cha Marekani katika eneo la Asia ya Magharibi.
Mnamo Juni 24, kupitia mashambulizi ya kujibu yaliyofanikiwa dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, Iran ilifanikiwa kuzuia mashambulizi hayo haramu.