Rais Pezeshkian: Vita vya kisaikolojia vya Marekani vinalenga kuvuruga usalama Asia Magharibi
-
Rais Pezeshkian na Bin Salman
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameonya kwamba harakati za kijeshi za Marekani katika Asia Magharibi ni sehemu ya juhudi zilizopangwa za kuyumbisha amani ya eneo hilo.
Rais Pezeshkian alitoa matamshi hayo jana jioni katika mazungumzo ya simu na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.
"Vitisho na operesheni za kisaikolojia za Wamarekani zinalenga kuvuruga usalama wa eneo la Asia Magharibi na hazitafanikisha chochote zaidi ya kuvuruga amani," Pezeshkian amemwambia Mwanamfalme Bin Salman.
Matamshi hayo yanafuatia kuwasili kwa meli ya kubeba ndege ya Marekani katika eneo hilo na mfululizo wa vitisho vinavyoongezeka kutoka Washington.
Wakati wa mazungumzo hayo ya simu, Rais Pezeshkian ameashiria ongezeko la uadui wa Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran tangu kuanza kwa utawala wake.
Ametaja mashinikizo ya kiuchumi, Vita vya Siku 12 dhidi ya Iran, na kuhusika moja kwa moja Marekani na washirika wake katika kuchochea ghasia za hivi karibuni za kigaidi ndani ya Iran, ambazo zilisababisha mauaji ya raia na askari usalama na vilevile uharibifu mkubwa wa mali ya umma, ikiwa ni pamoja na masoko na misikiti.
"Walidhani kwamba wangeweza kuigeuza Iran kuwa Syria au Libya nyingine," amesema Rais Pezeshkian na kusisitiza kuwa: "Walishindwa kutambua ukweli, asili na ukuu wa taifa la Iran. Uwepo wa watu wetu katika medani ulishinda njama zao," akimaanisha maandamano makubwa ya mamilioni ya Wairani kupinga ghasia kote Iran katika wiki zilizopita.
Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitishia kuishambulia Iran ikiwa eti itaua kile alichokiita "waandamanaji wa amani."
Siku chache tu baadaye, yaani Januari 8 na 9, makundi ya kigaidi yalianzisha wimbi la mashambulizi ya silaha dhidi ya vituo vya polisi, kambi za kijeshi na maeneo mengine nyeti, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya raia, katika miji kadhaa nchini Iran.
Maafisa wa Iran wanasema mashambulizi hayo ya vurugu yalikusudiwa kusababisha vifo vya watu wengi na kuvuruga utulivu katika miji mbalimbali kote nchini.
Pia wamekosoa mara kwa mara vyombo vya habari vya Magharibi kwa kusambaza ripoti nyingi za uongo kuhusu idadi ya waliouawa kwenye ghasia hizo na propaganda zao za kuhusisha serikali ya Iran na vifo hivyo.
Iran pia imeonya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itatoa "jibu la kujutisha" kwa kitendo chochote cha uchokozi, ikisisitiza kwamba taifa hili sasa lina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi kuliko hapo awali.