Shamkhani: Iran itashambulia ndani ya kitovu cha 'Israel' kulipiza kisasi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136118-shamkhani_iran_itashambulia_ndani_ya_kitovu_cha_'israel'_kulipiza_kisasi
Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, ameonya kwamba hatua yoyote ya uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu inaweza kuchochea majibu makali, ikiwemo mashambulizi yatakayopenya kwa kina ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ambayo yamepachikwa jina bandia la 'Israel'.
(last modified 2026-02-01T02:29:12+00:00 )
Feb 01, 2026 02:29 UTC
  • Admeri Ali Shamkhani
    Admeri Ali Shamkhani

Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, ameonya kwamba hatua yoyote ya uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu inaweza kuchochea majibu makali, ikiwemo mashambulizi yatakayopenya kwa kina ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ambayo yamepachikwa jina bandia la 'Israel'.

Admeri Ali Shamkhani, aliyewahi kuwa katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amesisitiza katika mahojiano na Televisheni ya al-Mayadeen ya  Lebanon kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina ufuatiliaji kamili wa mipango ya kioperesheni ya adui na iko tayari kwa matukio mapana na ya juu zaidi, yanayozidi mipaka ya baharini.

Mshauri huyo amesema kwamba “kipaumbele cha juu kabisa” kwa Iran ni kudumisha utayari kamili wa kuzuia tishio lolote, akitoa onyo kali kwamba “kitendo chochote kinachoashiria nia ya uhasama kutoka kwa adui kitajibiwa kwa hatua madhubuti, ya uwiano, na yenye uwezo wa kuzuia.”

Afisa huyo alionya pia kwamba upeo wa mapambano ya Iran haujazuiliwa kijiografia katika maeneo ya baharini pekee, na kwamba maandalizi tayari yamefanyika kwa matukio mapana na ya juu zaidi.

Akizungumzia ongezeko la uwepo wa majeshi ya kigeni katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, Shamkhani amesema kwamba uhamishaji huo wa vikosi hauashirii lazima kuwa na ubora wa kijeshi. Aidha amesema “nneo hili ni nyumbani kwa Iran,”  na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ina uelewa wa kina zaidi kuhusu jiografia yake, uwezo wake, na misingi yake ya ulinzi kuliko nguvu yoyote ya nje.

Kauli zake zilitolewa wakati mvutano ukiongezeka, kufuatia jaribio la Marekani na utawala wa Israel la kuanzisha uchokozi mpya dhidi ya Iran kwa kisingizio cha Jamhuri ya Kiislamu.

Marekani imeongeza  kiwango kikubwa uwepo wa kijeshi katika eneo, huku Rais Donald Trump akitoa vitisho vya mara kwa mara vya kulenga Jamhuri ya Kiislamu.

Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba watajibu kwa uthabiti dhidi ya tishio lolote linalolenga mamlaka na mipaka ya nchi.