Rais Pezeshkian aweka masharti ya mazungumzo na Marekani, 'hakuna vitisho, hakuna mashinikizo'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136210-rais_pezeshkian_aweka_masharti_ya_mazungumzo_na_marekani_'hakuna_vitisho_hakuna_mashinikizo'
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema amemwagiza waziri wa mambo ya nje kuendelea na mazungumzo na Marekani, alimradi yafanyika katika mazingira ya kuheshimiana na yasiyo na vitisho.
(last modified 2026-02-03T09:29:32+00:00 )
Feb 03, 2026 08:29 UTC
  • Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian
    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema amemwagiza waziri wa mambo ya nje kuendelea na mazungumzo na Marekani, alimradi yafanyika katika mazingira ya kuheshimiana na yasiyo na vitisho.

Katika mfululizo wa machapisho kwenye akaunti yake ya X leo Jumanne, Rais Pezeshkian amesema, amemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi kujibu pendekezo la Marekani la kufanya mazungumzo kufuatia maombi kutoka kwa "serikali rafiki katika eneo la Magharibi mwa Asia."

"Nimemwagiza Waziri wangu wa Mambo ya Nje, alimradi tu kuwe na mazingira yanayofaa—yasiyo na vitisho na matarajio yasiyo na msingi—kufuatilia mazungumzo ya haki na usawa, yanayoongozwa na kanuni za utu, busara na wepesi," ameandika Rais Pezeshkian na kuongeza: "Mazungumzo hayo yatafanyika ndani ya mfumo wa maslahi ya taifa letu."

Matamshi yake yanafuatia ripoti kwamba mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump wa Marekani, Steve Witkoff, na Araghchi wanatarajiwa kukutana Ijumaa ijayo mjini Istanbul.

Juhudi hizo za kidiplomasia zinakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka Asia Magharibi baada ya Marekani kutuma vikosi vya jeshi la majini katika eneo hilo.

Iran imeonya kwamba itajibu kwa nguvu hata hatua ndogo zaidi ya kijeshi ya Marekani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alionya Jumapili iliyopita kwamba vita vya kikanda vitazuka ikiwa Marekani itathubutu kushambulia Iran.

Iran imekataa katakata matakwa ya awali ya Marekani kama masharti ya makubaliano ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na kusitishwa kabisa urutubishaji wa madini ya urani nchini na kubana uwezo wake wa makombora.