Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu awapongeza wanamichezo wa Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza wanamichezo waliotwaa medali, wanamichezo wengine wote pamoja na makocha wa msafara wa wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walioshiriki kwenye mashindano ya Olimpiki ya Rio 2016.
Katika ujumbe wake huo kwa msafara wa wanamichezo waliorejea nchini kutoka kwenye mashindano ya Olimpiki ya Rio, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema: "Mashujaa mliolifurahisha taifa la Iran kwa kutwaa medali, mashujaa ambao walinyimwa haki yao kutokana na uamuzi usio wa haki, wanamichezo ambao thamani ya jitihada zao haipungui licha ya kutopata mafanikio, wanamichezo wanawake ambao wamejifaharisha mbele ya watu wote kutokana na nembo ya kujivunia ya vazi lao la mwanamke wa Kiirani, mwanamama shujaa aliyeung'arisha msafara kwa vazi kamili la Hijabu, makocha na wanamichezo wakongwe wa Iran, nasema karibuni na nakushukuruni nyote. Tunaijua thamani yenu".
Msafara wa wanamichezo wa Iran ulioshiriki kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika kwa muda wa majuma mawili mjini Rio de Janeiro nchini Brazil walifanikiwa kutwaa medali tatu za dhahabu, moja ya fedha na nne za shaba na kushika nafasi ya 25 katika mashindano hayo.
Katika mashindano ya Olimpiki yaliyopita ya mwaka 2012 ya mjini London, Uingereza, msafara wa wanamichezo wa Iran ulishika nafasi ya 17.../