Kiongozi Muadhamu: Kambi inayokabiliana na Iran ni ya makhabithi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i14134-kiongozi_muadhamu_kambi_inayokabiliana_na_iran_ni_ya_makhabithi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, adui anapaswa kufahamu kuwa, kama atajaribu kuishambulia Iran, atapata pigo kubwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 28, 2016 10:03 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Kambi inayokabiliana na Iran ni ya makhabithi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, adui anapaswa kufahamu kuwa, kama atajaribu kuishambulia Iran, atapata pigo kubwa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amesema hayo leo wakati alipoonana na makamanda na maafisa wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Khatamul Ambiya cha jeshi la Iran na huku akitilia mkazo suala la ulinzi wa anga ukiwa ni mstari wa mbele katika kukabiliana na mashambulizi ya aina yoyote ile amesema, kambi inayokabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ni kambi ya watu makhabithi, walaghai na wapinzani wa uhuru wa taifa la Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi nchini vinapaswa kujiimarisha kwa kila namna kwa ajili ya kukabiliana na adui huyu ambaye lengo lake kuu ni kutaka kudhoofisha uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu, na ifike mahala adui asiweze hata kufikiria kuivamia Iran.

 

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, azma, nia na uwezo wa nguvu kazi ni mambo muhimu ya kuweza kuondoa vizuizi na mapungufu yanayojitokeza na kuongeza kwamba: Kituo cha Ulinzi wa Anga ni moja ya mistari mikuu ya mbele vitani na inabidi thamani ya nafasi hiyo itunzwe na kufanyike jitihada za kila upande kwa kutumia azma, nia ya kweli na kutotetereka ili kudhoofisha nia ya adui ya kuishambulia Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uadui dhidi ya taifa la Iran na dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na uadui unaojulikana leo duniani baina ya nchi na mataifa mbalimbali. Ameongeza kuwa, kambi inayokabiliana na Iran kama vile kambi ya mabeberu au Uzayuni wa kimataifa ni kambi ya watu makhabithi, malaghai na wenye fikra za kidhulma ambayo uadui wao ni dhidi ya asili ya itikadi za kidini, uhuru na kutokubali kuburuzwa taifa la Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Amesema uadui wa kambi hiyo unadhihirishwa kwa sura tofauti na kuongeza kuwa: Uadui huo utaona siku moja unadhihirika kwa sura ya Marekani na siku nyingine kwa sura ya tawala za kidhalimu kama za Saddam, amma lililo muhimu ni kuwa, Iran inapaswa kuchukua misimamo na maamuzi sahihi na kuyafanyia kazi kivitendo kwa kutumia suhula na uwezo wake mwingi ilio nao pamoja na kuelewa vizuri zama zilizopo na mipango ya adui.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, kuzuka makelele mengi kuhusu mfumo wa kujilinda kwa mokombora wa S-300 au taasisi kama ya Fordow ni miongoni mwa mifano ya wazi ya ukhabithi wa adui wa taifa la Iran. Ameongeza kuwa: Mfumo wa kujilinda kwa makombora wa S-300 ni mfumo wa kujilinda na kujihami; si mfumo wa kushambulia, lakini pamoja na hayo Wamarekani wanafanya njama zao zote kuzuia Iran isifaidike na mfumo huo ambao hauna madhara kwa nchi yoyote ile.