Dakta Zarif: Hakuna ugaidi mzuri na mbaya; ugaidi upigwe vita na wote
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, walimwengu wote wanapaswa kusimama na kupambana na ugaidi na kwamba, hakuna ugaidi mzuri na mbaya.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Salahuddin Rabbani Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan na kusisitiza kwamba, Iran inapinga kugawanywa ugaidi katika makundi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya.
Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuenea vitendo vya ugaidi na vya kuchupa mipaka katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kwamba, walimwengu wote wanapaswa kusimama na kupambana na makundi yote yaliyochupa mipaka na ya kitakfiri.
Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo yake na Salahuddin Rabbani kwamba, Afhanistan ni nchi yenye umuhimu wa kipekee kwa Iran na kwamba, amani, usalama, utulivu na uthabiti wa nchi hiyo jirani ndio amani na utulivu wa Iran pia.
Kwa upande wake Salahuddin Rabban Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan ameshukuru ukarimu wa Wairani na kuashiria safari mbalimbali za viongozi wa Kabul mjini Tehran na kusema kuwa, safari hizi na mazungumzo ya mara kwa mara ya pande mbili ni jambo linalobainisha juu ya umuhimu wa Iran kwa serikali na wananchi wa Afghanistan.
Salahuddin Rabban Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan aliwasili mjini Tehran Jumatatu ya jana kwa ajili ya ziara rasmi hapa nchini ambapo mbali na Dakta Zarif ameshakutana na kufanya mazungumzo pia na Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.