Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika kubainisha tukio la Ghadir
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i15772-hotuba_ya_kiongozi_muadhamu_wa_mapinduzi_katika_kubainisha_tukio_la_ghadir
Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, jana alikutana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali kwa mnasaba wa Sikukuu ya Ghadir Khum ambapo mbali na kutoa mkono wa pongezi, heri na baraka kwa Waislamu alizungumzia umuhimu wa tukio la kihistoria la Ghadir katika pande tofauti.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 21, 2016 08:10 UTC
  • Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika kubainisha tukio la Ghadir

Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, jana alikutana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali kwa mnasaba wa Sikukuu ya Ghadir Khum ambapo mbali na kutoa mkono wa pongezi, heri na baraka kwa Waislamu alizungumzia umuhimu wa tukio la kihistoria la Ghadir katika pande tofauti.

Ayatullah Khamenei aliashiria baadhi ya tafsiri zilizotolewa kuielezea Sikukuu ya Ghadir kama "Idi Kubwa ya Kidini" na kueleza kwamba: Sababu ya kutolewa tafsiri hizo ni tukio muhimu sana lililotokea katika kadhia ya Ghadir ambalo ni kuainishwa kigezo na kanuni za utawala katika Uislamu. Kanuni hiyo ni Uimamu na Wilaya katika Jamii ya Kiislamu ambao ulitangazwa na Mtume SAW kwa amri ya Mwenyezi Mungu. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akihutubia hadhara ya wananchi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema, kudumisha umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ni moja ya nukta muhimu za kutukuka Ulimwengu wa Kiislamu na akasisitiza kwa kusema: "Kuchochea hisia za madhehebu zingine za Kiislamu kwa kutumia jina la Ushia, hakika yake ni "Ushia wa Kiingereza" ambao matokeo yake ni kujitokeza makundi habithi na mamluki vibaraka wa Marekani na Shirika la Ujasusi la Uingereza kama Daesh na An-Nusrah ambayo yamefanya jinai nyingi na angamizi katika eneo.

Matakfiri wa kundi la Daesh (ISIS)

Tukitupia jicho historia ya huko nyuma tutabaini kuwa katika zama tofauti za historia madola ya kinyonyaji yameusababishia Uislamu hasara na madhara makubwa; na historia yenyewe ni shahidi wa hayo. Kukabiliana na Uislamu kumefanywa kwa kutumia mbinu mbalimbali, na moja ya mbinu hizo ni kuingiza ushawishi kwenye fikra na mitazamo ya madhehebu za Kiislamu na kuzusha mifarakano baina ya madhehebu hizo.

Tokea tangu na tangu matatizo haya yametoa mwanya wa kujipenyeza maajinabi na kuwa chanzo cha kupotea mshikamano baina ya nchi za Kiislamu. Leo hii pia historia inajirudia. Kwani madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani ambayo yangali na malengo yale yale ya kikoloni yanataka kuzidhoofisha nchi za Kiislamu; hivyo yanautumia ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka ya aina ya Daesh kama wenzo wa kuzusha hitilafu na kuwaangamiza Waislamu.

Iran ya Kiislamu, leo hii imekuwa mlengwa namba moja wa maadui katika nyuga mbalimbali; kuanzia vita laini, mbinyo wa kiuchumi, vikwazo mpaka vitisho vya kushambuliwa kijeshi. Lengo la uhasama na uadui wote huo ni kutaka kuutoa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwenye mkondo wa utawala wa kidini na mhimili wa kukabiliana na mfumo wa kibeberu. Lengo linalofuatiliwa na maadui wa Iran ambao ni maadui wa Uislamu ni kuidhuru mihimili na nguzo za mfumo wa Kiislamu ambazo ni uadilifu na Wilaya. Hata hivyo njama hiyo imegonga ukuta kutokana Iran ya Kiislamu kushikamana na thamani za kidini, kuwa na irada thabiti na kuwepo vijana ambao ndio rasilimali kuu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Lakini pamoja na hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alikumbusha katika hotuba yake kuwa moja ya malengo ya adui ambalo lina umuhimu mkubwa katika wakati huu ni kuvuruga uchumi wa Iran ili kuzusha manung'uniko na kuwafanya wananchi wasiridhishwe na mfumo wa Kiislamu.

Marekani; kiranja wa mfumo wa ubeberu

Tukizingatia nukta hizi za msingi sambamba na uwezo mkubwa wa dini ya Uislamu tutabaini kuwa japokuwa adui ameshindwa katika njama zake nyingi lakini haipasi kughafilika na umuhimu wa kuwa na utayari unaohitajika kwa ajili ya kuulinda mfumo na thamani zake zinazofuata ilhamu ya utawala wa Wilaya ya haki ya Amirul Muuminin Ali (AS). Kuyazingatia malengo mbalimbali likiwemo la uchumi wa muqawama katika wakati huu kuna umuhimu kwa kiwango sawa na kujiweka tayari kijeshi kwa ajili ya kuzuia vitisho na kutoa jibu kwa yeyote atakayejaribu kufanya uchokozi. Ni kwa sababu hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alisistiza mara kwa mara katika hotuba yake juu ya umuhimu wa kuthibiti uchumi wa muqawama na kueleza kwamba katika mazingira kama haya jukumu la Serikali, Bunge, wakuu wa vyombo mbalimbali pamoja na wananchi wote ni kujipanga na kuchukua hatua ambazo zitakabiliana na malengo ya adui.../