Iran: Umoja wa Mataifa usiegemee upande wowote katika mgogoro wa Syria
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika amesema kuwa, katika kuleta amani na usalama wa kimataifa, Umoja wa Mataifa haupaswi kuegemea upande wowote katika mgogoro wa Syria.
Hossein Jaber Ansari amesema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari baada ya kukutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Staffan de Mistura, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria.
Jaber Ansari amesisitiza kuwa, ni jambo la muhimu mno kwa Umoja wa Mataifa sambamba na kusaidia kutumwa misaada ya kibinadamu nchini Syria uchukua hatua za maana na zenye taathira katika kupambana na ugaidi na hivyo kuandaa mazingira mazuri ya kuondolewa nchi hiyo katika mgogoro inaokabiliwa nao.
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika amesisitiza kuwa, kuhifadhiwa umoja wa ardhi ya Syria ni jambo muhimu sana na wakati huo huo zuchukuliwe hatua yoyote muhimu yenye lengo la kupatiwa ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Staffan de Mistura, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria ametakwa kuweko fikra za pamoja za Tehran na Umoja wa Mataifa katika kuandaa mipango ya kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro inaokabiliwa nao hasa kwa kuzingatiwa nafasi muhimu iliyonayo Iran.