Kiongozi Muadhamu alionya Baraza la Congress la Marekani
(last modified Sun, 27 Nov 2016 16:59:31 GMT )
Nov 27, 2016 16:59 UTC
  • Kiongozi Muadhamu alionya Baraza la Congress la Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelionya Baraza la Congress la Marekani akisisitiza kuwa, hatua yoyote ya kuvirudisha vikwazo ambavyo muda wake umeisha ni uwekaji wa vikwazo vipya na ni uvunjaji wa makubaliano.

Ayatullah Khamenei amesema hayo leo kwa mnasaba wa kumbukumbu za kikosi cha majini cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaani tarehe 27 Novemba, wakati alipoonana na makamanda na maafisa wa kikosi hicho.

Vile vile amegusia mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 yaliyomalizika kwa kufikiwa makubaliano ya JCPOA na kutahadharisha mpango wa Baraza la Congress la Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya Iran huku likidai kuwa hivyo si vikwazo vipya bali ni kurefusha tu vikwazo. Amesema, hakuna tofauti yoyote baina ya kuweka vikwazo vipya na kuendeleza vikwazo ambavyo muda wake umeisha, na kwamba hatua hiyo ya kurefusha muda wa vikwazo ni uvunjaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi hilo la 5+1.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya harakati zake za kukagua vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu.

 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei vile vile amezungumzia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kikosi cha majini cha jeshi la Iran kwenye nyuga tofauti kuanzia nguvukazi ya watu hadi kwenye uongozi na teknolojia za kisasa zinazotumika kwenye jeshi hilo na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kuondolewa mapungufu yote kwa hima ya hali ya juu na kutokwamishwa na mapungufu na vizuizi vyovyote vinavyojitokeza.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema, Iran ina uzoefu mkubwa sana wa harakati za baharini kutokana na kuwa na mipaka mikubwa ya majini hivyo uwezo na nguvu za kikosi cha majini cha jeshi la Iran kinapaswa kuwa katika hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa na Admeri Habibullah Sayyari, Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Tarehe 27 Novemba ni siku ya kukumbuka hamasa kubwa ya maafisa wa boti ya makombora ya Peykan ambapo karibu miezi miwili baada ya kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jeshi la baharini la Iran lilifanya operesheni  ya kishujaa katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuweza kulishinda jeshi la Iraq. Katika operesheni hiyo, jeshi la Iran liliangamiza askari wengi wa Iraq na kuwasababishia hasara kubwa na kufanikiwa kuidhibiti kikamilifu Ghuba ya Uajemi. Siku hiyo inatambuliwa hapa nchini Iran kuwa ni Siku ya Jeshi la Majini.