Ayatullah Subhani asisitiza umoja wa Waislamu ili kung'oa mizizi ya utakfiri
(last modified Mon, 19 Dec 2016 14:46:58 GMT )
Dec 19, 2016 14:46 UTC
  • Ayatullah Subhani asisitiza umoja wa Waislamu ili kung'oa mizizi ya utakfiri

Mmoja wa marajii taqlidi katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran amesisitiza juu ya udharura wa kuungana na kuwa kitu kimoja maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu ili kutokomeza mizizi ya matakfiri duniani.

Akizungumza leo katika mkutano na maulamaa wa Kishia na Kisuni wa Uingereza katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini, Ayatullah Jaafar Subhani ameeleza kusikitishwa na mauaji yanayofanywa na makundi ya kigaidi na kitakfiri dhidi ya Waislamu kwa jina la Uislamu na kueleza kuwa, maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu wanapasa kuchukua hatua kivitendo kuzuia kutokea migawanyiko kati ya Waislamu na kuwataka wazungumzie kuhusu Tauhidi na shirki. 

Ayatullah Jaafar Subhani Marja Taqlidi wa Qum ambaye ametaka kutokomezwa mizizi ya utakfiri

Ayatullah Subhani amesema kuwa Qur'ani Tukufu inawahutubu Waislamu kuwa wamoja na kuongeza kuwa, Mwenyezi Mungu, kitabu na kibla cha Waislamu ni kimoja na kwamba, kushikamana na suala la umoja ni wenzo utakaowanasua Waislamu katika shimo la ujahilia na kuangamia. Marjaa taqlidi huyo katika mji mtakatifu wa Qum ameongeza kuwa, matakfiri na Mawahabi nchini Saudi Arabia wamesababisha kufundishwa ugaidi katika shule za kidini na hivyo kuasisi mbegu za chuki na uhasama katika nyoyo za watoto.