Jan 10, 2017 03:46 UTC
  • Rais wa Algeria: Iran imepoteza kiongozi shujaa na mwana mwaminifu

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametuma salamu za rambirambi kwa taifa la Iran kutokana na kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu hapa nchini, Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani.

Katika ujumbe wake uliotumwa kwa Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Bouteflika amesema, taifa na serikali ya Algeria inatoa mkono wa pole kwa taifa na serikali ya Iran kutokana na kifo cha Ayatullah Rafsanjani.

Rais wa Algeria amesifu misimamo ya kishujaa ya Rafsanjani na jitihada zake za kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza mmoja kati ya watoto wake waaminifu ambaye alisabilia maisha yake kwa ajili ya kuhudumia Iran na kuilinda nchi katika mazingira na vipindi vyote vigumu.

Ayatullah Rafsanjani

Rais wa Algeria ameongeza kuwa, historia inatoa ushahidi kuhusu misimamo ya kishujaa na msaada wa Ayatullah Rafsanjani kwa ajili ya kulinda umoja na mshikamano wa Kiislamu.

Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani alifariki dunia juzi usiku akiwa na umri wa miaka 82.

Jeneza lenye mwili wa Ayatullah Hashemi Rafsanjani

Miongoni mwa nyadhifa alizowahi kuzishika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Kaimu Amiri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ulinzi wa Taifa na nafasi aliyoishika hadi kifo chake ya Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.  

Tags