Shamkhani asisitiza kuheshimiwa misingi ya demokrasia huko Syria
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa jitihada zinazofanywa na baadhi ya nchi ikiwemo Marekani kwa ajili ya kuamua mustakbali wa Syria ni kinyume na misingi ya demokrasia na haki ya mataifa ya kujiainishia mustakbali wao.
Ali Shamkhani amesisitiza kuwa kuiunga mkono Syria na rais halali wa nchi hiyo Bashar al Assad kunajiri katika fremu ya stratejia ya Iran kwa minajili ya kusimamia harakati ya muqawama na kupambana na ugaidi. Shamkhani amesema demokrasia iliyopo Syria ni bora kuliko ile inayoshuhudiwa katika nchi zinazoungwa mkono na Marekani na kwamba Rais Bashar Assad anaungwa mkono vyema huko Syria. Amesema kwa mtazamo wa wananchi wa Syria, Rais Assad ameweza kusimama kidete mkabala na mgogoro ulioiathiri nchi hiyo.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa ushindi uliopatikana katika mji wa Halab yaani Aleppo umefichua wazi siri zilizo nyuma ya pazia kuhusu misaada ya moja kwa moja ya baadhi ya nchi kwa harakati ya ugaidi. Ali Shamkhani amesema kuwa, kuparaganyika mfumo uliopo katika eneo ni pigo kwa nchi zote na ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa nchi kama Uturuki na Saudi Arabia zinapasa kuweka wazi malengo yao; hii ni kwa sababu nchi hizo pia hazitasalimika kwa kuwa ni miongoni mwa wanaoshikia bango mpango wa nchi za Magharibi wa kutaka kuligawa eneo hili.