Nabih Berri: Nchi za Kiislamu zifunge balozi zao zilizoko Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25452-nabih_berri_nchi_za_kiislamu_zifunge_balozi_zao_zilizoko_marekani
Spika wa Bunge la Lebanon ameziasa nchi za Kiislamu zifunge balozi zao zilizoko Marekani kulalamikia mpango wa Washington wa kutaka kuhamishia ubaloizi wake ulioko Israel huko Quds Tukufu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 21, 2017 13:58 UTC
  • Nabih Berri: Nchi za Kiislamu zifunge balozi zao zilizoko Marekani

Spika wa Bunge la Lebanon ameziasa nchi za Kiislamu zifunge balozi zao zilizoko Marekani kulalamikia mpango wa Washington wa kutaka kuhamishia ubaloizi wake ulioko Israel huko Quds Tukufu.

Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon ameyasema hayo leo katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina unaofanyika hapa mjini Tehran na kubainisha kuwa, umefika wakati nchi za Kiislamu zifunge mara moja balozi zao zilizoko Marekani kutokana na hatua ya Washington ya kuunga mkono sera za utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwemo ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, licha ya azimio la kimataifa lililopinga unyakuzi huo.

Mkutano wa Sita wa Mimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina

Berri amesema azma ya Marekani ya kutaka kuuhamishia ubalozi wake mji wa Baitul Muqaddas ni uchokozi wa wazi unaonuia kuvurugu usalama si tu katika eneo bali kote duniani.

Katika kampeni zake za uchaguzi na baada ya kushinda uchaguzi wa rais, Rais Donald Trump wa Marekani amemuahidi Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kwamba serikali ya Washington itauhamishia ubalozi wake Beitul Muqaddas kutoka Tel Aviv.

Matamshi hayo ya Trump yamekabiliwa na radiamali kali ya viongozi wa Palestina na wa nchi nyingine duniani. Sheikh Akrama Sabri, Khatibu wa Masjidul Aqswa hivi karibuni alilaani vikali hatua ya kutaka kuhamishiwa ubalozi wa Marekani mjini Beitul Muqaddas na kuongeza kuwa hatua hiyo sio tu kuwa ni kutangaza vita dhidi ya Wapalestina bali pia ni kutangaza vita dhidi ya Waislamu wote duniani.