Ripoti: Trump, UAE wanakula njama ya kuitenganisha Russia na Iran
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) uliandaa mkutano wa siri mapema mwaka huu kati ya mwakilishi wa rais mteule wakati huo wa Marekani Donald Trump na mpambe wa Rais Vladimir Putin wa Russia ili kufanikisha diplomasia ya mlango wa nyuma baina ya pande mbili.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na toleo la jana la Gazeti la Washington Post. Maafisa wa Marekani, Ulaya na wa Kiarabu wameliambia gazeti hilo kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati ulikubali kusimamia mazungumzo katika visiwa vya Seychelles ili kujaribu kuishawishi Russia ipunguze uhusiano wa karibu ilionao na Iran.
Kwa mujibu wa maafisa ambao hawakutaKa kutajwa majina yao, Mrithi wa Imarati ya Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahyan alifanya safari kwa siri mjini New York mwezi Desemba mwaka jana na kufanya mazungumzo na aliyekuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, Michael Flynm, mkwe wa rais huyo wa Marekani Jared Kushner na Mkuu wa Stratijia katika Ikulu ya White House Steve Bannon.
Zayed pamoja na kaka yake ambaye ni mshauri wa usalama wa taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu, walijadili na maafisa hao wa serikali ya Trump njia za kutumia ili kuifanya Russia ikate uhusiano wa karibu ilionao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa maafisa hao, Zayed alifanya mazungumzo mara zisizopungua mbili na Rais wa Russia katika mwaka uliopita wa 2016 na kujaribu kumshawishi awe na ushirikiano wa karibu na Imarati na Saudi Arabia na kupunguza uhusiano wake na Iran.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali iliyopita na ya sasa ya Marekani, Washington na Abu Dhabi zimeshughulishwa mno na Iran na kuongezeka ushawishi wake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hata hivyo balozi wa zamani wa Marekani nchini Russia Michael McFaul anaamini kuwa si rahisi kwa serikali ya Moscow kufuata muelekeo huo kwa sababu haipati maslahi yoyote kwa kufanya hivyo na vilevile kutokana na uhusiano wake wa muda mrefu na Iran ambayo ni muitifaki wake katika kupambana na magaidi nchini Syria…/