Iran yaangamiza magaidi wanne wa ISIS na kunasa silaha na bendera
Maafisa wa usalama kusini mwa Iran wamefanikiwa kuwaangamzia magaidi wanne wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh sambamba na kunasa silaha walizokuwa nazo pamoja na bendera ya kundi hilo la kigaidi.
Akizungumza na waandishi habari jana Jumatatu, Mkuu wa Polisi katika mkoa wa Hormozgan Azizullah Maleki amesema magaidi hao waliuawa katika mapigano na maafisa wa usalama.
Amesema maafisa wa polisi katika eneo hilo wamekuwa wakifuatilia nyendo za magaidi hao na baada ya kubaini malengo yao, kulitekelezwa oparesheni ya kukabiliana nao. Amesema oparesheni hiyo ilifanyika katika eneo la milimani karibu na wilaya ya Roudani mkoani humo. Amesema magaidi hao walikuwa na bunduki nne, risasi 112, mada za milipuko pamoja na bendera ya ISIS.
Aidha imebainika kuwa magaidi wawili kati ya waliouawa walikuwa ni raia wa kigeni huku utambulisho wa waliosalia ukiwa bado haujabainika. Jumatano iliyopita watu 17 waliuawa shahidi katika mji mkuu wa Iran wakati magaidi waliposhambulia bunge la Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA.
Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na hujuma hiyo. Magaidi watano walioshiriki katika hujuma hiyo waliuawa huku wengine karibu 60 waliohusika wakiwa tayari wameshakamatwa. Aidha kinara wa hujuma hiyo ya Jumatano aliyekuwa ametorokea nchi jirani amesakwa na hatimaye kuangamizwa na vikosi vya usalama vya Iran .