Matamshi ya uingiliaji ya Tillerson; kilele cha kuchanganyikiwa Marekani mbele ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameonyesha msimamo ambao ni wa uhasama na uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo hivi sasa inaelekea kutimiza miaka arubaini ya uhai wake.
Suala hilo linaonyesha wazi kwamba watawala wa Marekani wangali wanafuatilia kwa nguvu zao zote ndoto isiyotimia na ambayo wamekuwa wakiifuatilia tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran bila ya mafanikio yoyote, na Inshallah hawatafanikiwa kabisa. Katika matamshi yanayokinzana na misingi yote ya sheria za kimataifa, yasiyokubalika na yanayopaswa kulaaniwa na kila mtu, aliyoyatoa hapo siku ya Jumatano, Rex Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema kuwa nchi hiyo inaunga mkono watu walio ndani ya Iran ambao wako tayari kuusaidia utawala wa Washington kubadilisha serikali ya Iran kwa njia ya amani. Bila shaka matamshi hayo yanathibitisha wazi kwamba Marekani imechanganyikiwa na kushindwa na mfumo wa wananchi shupavu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mbali na hayo, matamshi hayo yasiyo na msingi na ya kipumbavu ya Tillerson yanapingwa vikali na taifa la Iran. Moja ya malengo ya siku zote ya Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kuupindua Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo za kijeshi na za mapinduzi laini, lakini imeshindwa kabisa kufikia lengo lake hilo ovu kutokana na kutofahamu vyema masuala ya ndani ya Iran.
Kabla na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani imekuwa ikifanya kila inaloweza ili kuingilia moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja maamuzi ya wananchi wa Iran. Mapinduzi ya mwaka 1953 nchini Iran ni mfano wa wazi wa uingiliaji wa Marekani dhidi matakwa ya wananchi wa Iran, ambao kwa kutaifisha sekta ya mafuta nchini walithibitisha wazi kuwa hawakutaka kuchukuliwa maamuzi na wageni. Ushirikiano wa mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza ulipelekea kupinduliwa serikali ya Dakta Musaddiq, na uchocheaji wa nchi mbili hizo za kigeni katika mapinduzi hayo uko wazi kwa kila mtu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uadui na uhasama wa Wamarekani dhidi ya taifa la Iran ilidhihiri wazi zaidi, ambapo walianza kuyalenga moja kwa moja mapinduzi hayo. Operesheni ya Tabas, kuanzishwa vita vya kulazimishwa vya utawala wa Kibaathi wa Saddam dhidi ya Iran, kuuawa kigaidi viongozi wa kisiasa na kidini nchini, kushirikiana na kundi la kigaidi la Munafiqeen dhidi ya wanamapinduzi na vikwazo tofauti vya kiuchumi ni mbinu ambazo Wamarekani walizitumia baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuilazimisha Iran isalimu amri lakini bila ya mafanikio yoyote.
Wananchi wa Iran daima wamekuwa wakishiriki katika minasaba na matukio muhimu ya kulinda Mapinduzi ya Kiislamu, kukiwemo kushiriki kwenye chaguzi na maandamano ya tarehe 22 Bahman ambayo ni tarehe ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na hivyo kutoa jibu muwafaka kwa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Wananchi hayo walithibitisha tena kuchukizwa kwao na Wamarekani kwa kushiriki kwa kishindo na kwa mamilioni katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika hapa nchini tarehe 19 mwezi Mei uliopita. Marekani daima imekuwa ikifanya njama za kuzua fitina na mifarakano miongoni mwa Wairani walio na umoja na mshikamano wa kitaifa ili wachukie na kujitenga na mfumo wao wa Kiislamu, ndoto ambayo imeshindwa kuifikia hadi leo.
Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009, Marekani ilishirikiana na watu walio dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na waliopotoshwa na propaganda za nchi hiyo kwa kudai kwamba udanganyifu ulifanyika katika uchaguzi huo, ili kujaribu kuzua mgawanyiko kati ya wananchi na Mfumo, lakini ikashindwa vibaya katika njama hiyo kutokana na mwamko mkubwa wa wananchi.
Ni wazi kuwa umoja, busara, utambuzi mzuri wa wananchi kuhusu adui mkuu wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na nguvu zinazoongezeka kila siku za Iran ya Kiislamu ni mambo ambayo yameifanya Marekani ishindwe kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu na bila shaka matamshi ya kichochezi na ya uingiliaji ya Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani yanaweza kutafsiriwa tu katika mtazamo huo. Kwa maneno ya Bahram Qassimi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, 'kuchanganyikiwa', 'kuathirika na madai yasiyo na msingi' na 'kukimbia ukweli' ni mambo yanayoonekana wazi katika siasa za nje za serikali mpya ya Marekani.