Kiongozi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko imara, itatoa pigo kwa adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30656-kiongozi_jamhuri_ya_kiislamu_ya_iran_iko_imara_itatoa_pigo_kwa_adui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara na kwamba taifa la Iran litatoa pigo kwa adui.
(last modified 2026-02-22T09:20:04+00:00 )
Jun 19, 2017 03:53 UTC
  • Kiongozi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko imara, itatoa pigo kwa adui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara na kwamba taifa la Iran litatoa pigo kwa adui.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei aliyasema hayo Jumapili mjini Tehran alipokutana na familia  za mashahidi walinzi wa Haram Takatifu na vikosi vya usalama vinavyolinda mipaka ya nchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vitisho na uhasama katika kauli za wakuu wa Marekani siku za hivi karibuni na kusema: "Watawala wa Marekani tokea mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu daima wamekuwa wakifuatilia njama ya kuubadilisha mfumo wa Kiislamu wa Iran lakini hawataweza kulipa taifa la Iran pigo bali ni taifa la Iran litakalowapa pigo."

Kiongozi Muadhamu ameashiria kuendelea kubakia imara mfumo wa Kiislamu wa Iran pamoja na kuwepo hujuma za  maadui na kusema: "Matamshi ya kijuba ya rais wa Marekani si jambo jipya. Hii ni kwa sababu tokea mwanzo wake, Mfumo wa Kiislamu umekuwa ukikabiliwa na njama mbali mbali lakini wanaolitakia mabaya taifa la Iran hawawezi kufanya lolote."

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: "Wakati Mfumo wa Kiislamu ulikuwa bado ni mche maadui hawakuweza kuupa pigo seuze sasa ambapo mfumo huu umekuwa mti imara."

Kiongozi Muadhamu akihutubua hadhara

Kiongozi Muadhamu ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya wakuu wa Marekani kuhusu njama zao za kubadilisha Mfumo wa Kiislamu wa Iran na kusema katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, wamekuwa wakipanga njama za kuubadulisha mfumo wa Kiislamu lakini njama zao hizo zimekuwa zikigonga mwamba na hali itaendelea kuwa hivyo katika siku za usoni.

Ayatullah Khamenei amewataja wakuu wapya katika Ikulu ya White House kuwa wanagenzi wasio na uzoefu na kusema: "Watawala wa Marekani tokea mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa wakijaribu kuuangusha mfumo wa Kiislamu lakini watu waliokuwa na ndoto hiyo walienda nayo kaburuni na hali itaendelea kuwa hivyo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema usalama uliopo hivi sasa nchini Iran ni kutokana na jitihada za Walinzi wa Haram Takatifu na huku akiwapongeza na kuwaenzi mashahidi Walinzi wa Haram amesema: "Iwapo si hawa mashahidi Walinzi wa Haram, leo tungekuwa tunapigana na waeneza fitina, makhabithi na maadui wa Ahul Bayt AS katika miji ya Iran. Hii ni kwa sababu walikuwa wanalenga kutumia mipaka ya Iraq kuingia Iran lakini tumewazuia na wameangamizwa na hivi sasa pia nchini Iraq na Syria wanaelekea kuangamizwa."