Saudia yashindwa kuishawishi OIC kutoa azimio dhidi ya Iran
Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kisiasa na Usalama wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, pendekezo la Saudia la kuingizwa kipengee cha kuilaani Iran katika taarifa ya mwisho ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC limetupiliwa mbali na wajumbe wa kikao hicho.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Gholam-Hossein Dehghani akiashiria njama zilizofanywa na Saudi Arabia za kuwashawishi mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa OIC kuingiza kipengee ya kuilaani Iran katika tamko lao la mwisho la kikao chao cha nchini Kodivaa na kuongeza kuwa, njama hizo za Riyadh za kutaka nchi za Kiislamu ziunge mkono tamko la Riyadh, zinakwenda kinyume na moyo na msingi wa hati inayounda Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ambayo inasisitizia mno umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu na kutatua changamoto za ulimwengu wa Kiislamu.
Dehghani ameongeza kuwa, kufanya njama dhidi ya Iran ndilo lililokuwa lengo kuu la Marekani na Saudi Arabia katika kikao hicho cha OIC lakini nchi za Kiislamu zinapaswa kupuuza njama hizo kwani shabaha ya Marekani na Saudia ni kuonesha uadui dhidi ya wananchi wa Palestina, wakati lengo kuu la kuasisiwa OIC lilikuwa ni kulitetea na kulihami taifa la Palestina.
Itakumbukwa kuwa, Saudia na Marekani zilidai kupitia tamko la Riyadh lililotolewa tarehe 21 Mei 2017 baada ya Saudia kukusanya baadhi ya nchi za Kiarabu katika mkutano uliohudhuriwa pia na rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa eti Iran inahatarisha usalama wa eneo hilo.
Kikao cha 44 cha mawaziri wa mambo ya nje wa OIC kimefanyika mjini Abidjan, Ivory Coast chini ya kaulimbiu ya "Vijana, amani na ustawi duniani."