Iran yazindua utengenezaji wa kombora jipya la anga la Sayyad-3
Uzalishaji wa kombora la anga la masafa marefu la Sayyad-3 umezinduliwa leo katika hafla iliyohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi hapa nchini.
Uzalishaji wa kombora hilo lililotengenezwa na wataalamu wa hapa nchini umefanyika leo katika sherehe iliyohudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi akiwemo Waziri wa Ulinzi, Meja Jenerali Hussein Dahqan na Kamanda wa Kituo cha Jeshi la Anga cha Khatamul Anbiya (saw), Farzad Ismaili, na baadhi ya makombora hayo tayari yamekabidhiwa kwa Jeshi la Anga.
Waziri wa Ulinzi wa Iran Meja Jenerali Dahqan amesema kuwa, stratijia ya wizara hiyo ni kuimarisha na kusasisha uwezo wa makombora ya anga ya Iran katika masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu na kwamba kombora la Sayyad-3 lina uwezo wa kutungua shabaha angani kutokea umbali wa karibu kilimota 120.
Meja Jenerali Hussein Dahqan ameongeza kuwa, kombora la anga la Sayyad-3 limetengenezwa kwa mujibu wa vigezo vya teknolojia mpya kabisa duniani na linaweza kukabiliana na kutungua ndege za kivita zisizoonekana na rada, ndege zisizo na rubani, makombora ya cruise, helikopta na kadhalika.
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa, wizara hiyo itaendelea kuimarisha uwezo wa jeshi la Iran kwa nguvu zake zote.