Qassemi: Iran itaendeleza mipango yake ya makombora kwa nguvu zake zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32450-qassemi_iran_itaendeleza_mipango_yake_ya_makombora_kwa_nguvu_zake_zote
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran ina haki ya kutoa majibu mwafaka dhidi ya hatua ya Marekani na kwamba, itaendelea mbele na mipango yake ya makombora.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 29, 2017 22:35 UTC
  • Qassemi: Iran itaendeleza mipango yake ya makombora kwa nguvu zake zote

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran ina haki ya kutoa majibu mwafaka dhidi ya hatua ya Marekani na kwamba, itaendelea mbele na mipango yake ya makombora.

Akizungumza hapo jana Jumamosi, Bahram Qassemi ameashiria hatua ya chuki ya hivi karibuni ya Marekani ya kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran na kusema kuwa, sera za Iran katika uwanja wa masuala ya kijeshi na makombora ziko wazi na kwamba watu wengine hawana haki ya kuingilia suala hili.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, sera za kiulinzi na za makombora za Iran ni kwa ajili ya kujihami taifa hili na kusaidia amani, uthabiti na usalama wa Mashariki ya Kati na katu si tishio kwa majirani na nchi nyingine.

Roketi la kubeba satalaiti la Simorgh

Bahram Qassemi ameashiria vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, hatua hiyo imejaa chuki na uadui na ni ya kulaaniwa na imefanyika kwa ajili ya kudhoofisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo kimsingi ni makubaliano ya pande kadhaa na ya kimataifa.

Aidha Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeashiria tuhuma za Marekani dhidi ya Tehran kwamba, inaunga mkono ugaidi na kusema bayana kwamba, taifa hili limefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kupambana na ugaidi, kinyume na Marekani ambayo inapinga amani na uthabiti wa Mashariki ya Kati kwa hatua yake ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.