Aug 17, 2017 02:38 UTC
  • Iran yalaani shambulio la kigaidi lilioua na kujeruhi zaidi ya 100 Nigeria

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la kigaidi lililosababisha mauaji ya makumi ya watu nchini Nigeria usiku wa kuamkia jana Jumatano.

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema kuna udharura wa kuwepo jitihada za kitaifa, kieneo na kimataifa katika kukabiliana na jinamizi la ugaidi.

Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo, Qassemi amesema jamii ya kimataifa ina kibarua kikubwa na safari ndefu ya kutokomeza harakati za kigaidi duniani, na hilo halitafanikiwa bila ushirikiano. 

Watu 27 waliuawa katika mji wa Medjugorje, kaskazini mashariki mwa Nigeria na wengine 83 kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi lililotekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Sehemu ya hujuma za kigaidi za Boko Haram nchini Nigeria

Vyombo vya usalama vya Nigeria vinaripoti kuwa, shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na watu watatu akiwemo mwanamke mmoja, ambao walijilipua wenyewe kwenye lango la kuingilia kambi ya wakimbizi katika kijiji cha Konduga karibu na mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno, eneo ambalo ni ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haramu.

Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya watu 12 kuuawa kusini mashariki mwa Nigeria na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu waliokuwa na silaha kuvamia kanisa moja na kuanza kuwamiminia watu risasi watu waliokuwamo ndani ya kanbisa hilo.

Tags