Ayatullah Larijani: Wamagharibi hawana nia ya kuutokomeza ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33464-ayatullah_larijani_wamagharibi_hawana_nia_ya_kuutokomeza_ugaidi
Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amesema kuwa, ulimwengu wa Magharibi hauna azma ya dhati ya kuutokomeza ugaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 22, 2017 02:41 UTC
  • Ayatullah Larijani: Wamagharibi hawana nia ya kuutokomeza ugaidi

Mkuu wa Idara ya Mahakama nchini Iran amesema kuwa, ulimwengu wa Magharibi hauna azma ya dhati ya kuutokomeza ugaidi.

Ayatullah Sadeq Amoli Larijani amesema kuwa, katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilaani mauaji ya kila namna, Ulaya na Marekani  zimekuwa zikiugawa ugadi katika makundi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya.

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hayo jana katika kikao na maafisa wa ngazi za juu wa Mahakama hapa nchini ambapo aliashiria mashambulio ya hivi karibuni ya kigaidi huko Barcelona nchini Uhispania na kusisitiza kwamba, ulimwengu wa Magharibi hauna nia ya kuutokomeza ugaidi bali umekuwa ukivitumia vitendo vichafu vya ugaidi kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine.

Jengo la Idara ya Bunge la Iran lilishambuliwa na wanachama wa Daesh Juni mwaka huu

Ayatullah Larijani amesema kwamba, dini ya Uislamu ikiwa mlinganiaji wa uhuru na haki za binadamu ulimwenguni, inapinga vikali kuuawa watu wasio na hatia yoyote.

Amesema kuwa, hii leo Rais Donald Trump wa Marekani anautuhumu Uislamu kwamba, eti unaunga mkono ugaidi, ambapo miamala kama hii ya kindumakuwili ndio inayopelekea kutong'olewa mizizi ya ugaidi duniani. 

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama amesema pia kuwa, katika kipindi cha miaka yote hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa muathiriwa  mkubwa wa ugaidi na hii leo, taifa hili liko mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi nchini Syria, Lebanon na Iraq.