Kiongozi Muadhamu ashiriki katika kuuaga mwili wa shahid Hojaji
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alfajiri ya leo Jumatano amekwenda katika Msikiti wa Imam Husain AS hapa Tehran na kuusomea Faatiha mwili mtoharifu wa shahid Mohsen Hojaji, aliyeuliwa shahidi na magaidi wa Daesh wakati akilinda Haram ya mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Zaynab al Kubra AS nchini Syria.
Mtandao wa habari wa Kiongozi Muadhamu wa Mapindizi ya Kiislamu umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, katika mahojiano aliyofanyiwa baada ya kumsomea Faatiha shahid huyo, Ayatullah Khamenei amemsifu shahid Hojaji kwa kujitolea kwake katika njia ya Mwenyezi Mungu na kumuomba Allah ampandishe daraja za juu za utukufu kama ambavyo pia amemuomba Mwenyezi Mungu azidishe subira na uvumilivu katika nyoyo za watu wa familia yake.
Shughuli ya kuuaga na kuusindikiza mwili ya shahid Mohsen Hojaji inafanyika leo hapa Tehran na baadaye mwili wake utapelekwa kijijini kwao katika mkoa wa Isfahan wa katikati mwa Iran kwa ajili ya maziko hiyo kesho Alkhamisi.
Tarehe 9 Agosti 2017, kundi la kigaidi la Daesh lilimuua shahidi kijana huyo muumini ambaye kwa mapenzi yake makubwa kwa watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW alikwenda nchini Syria kulinda haram za watukufu hao zisinajisiwe na magenge ya kigaidi kama vile Daesh.
Makundi ya kigaidi hasa Daesh (ISIS) hayaheshimu maeneo matakatifu ya Waislamu kama vile maeneo ya ibada ya mawalii wa Mwenyezi Mungu likiwemo eneo la ibada la Nabii Sheth AS ambalo magaidi wa Daesh waliliripua kwa mabomu huko Iraq na makaburi ya maswahaba wa Bwana Mtume pamoja na haram za wajukuu wa Mtume katika nchi za Iraq na Syria. Watu waliova kidini kutoka maeneo tofauti wameelekea katika nchi za Iraq na Syria kwenda kulinda maeneo hayo matakatifu ya mawalii wa Mwenyezi Mungu yasinajisiwe na maadui wa Uislamu.