Oct 09, 2017 02:30 UTC
  • Iran imechukua hatua imara kukabiliana na biashara haramu ya mihadarati

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi la Iran amesema ili kuwepo mafanikio katika vita dhidi ya biashara haramu ya mihadarati kunahitajika mikakati endelevu ya kimataifa na bajeti ya kutosha.

Meja Jenerali Mumini, ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran alipokutana na waambata wa kijeshi wa balozi za kigeni mjini Tehran na kuongeza kuwa, biashara haramu ya madawa ya kulevya ni tatizo kubwa duniani kwani madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa za kulevya yanazitia wasiwasi nchi nyingi duniani.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Iran ameongeza, kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua imara kukabiliana na tatizo la mihadarati na kwamba Iran peke yake haiwezi kabiliana na tatizo hili, hivyo kuna haja ya kuwepo jitihada za pamoja za kimataifa.

Amesema ushirikiano wa kimataifa katika uga wa vita dhidi ya mihadarati mbali na kuwaangamiza wanaosafirisha mihadarati pia utasaidia jitihada za kukabiliana na vinara wa biashara hiyo ambao wanapata faida kubwa za kifedha.

Mashamba ya Mihadarati nchini Afghanistan

Meja Jenerali Mumini amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitasitisha vita vyake dhidi ya mihadarati na hadi sasa imepata mafanikio katika uga huo na kwamba dunia nzima inanufaika na hatua zilizochukuliwa na Iran katika uwanja huo.

Tags