Oct 27, 2017 04:10 UTC
  • Qassemi: Ripoti ya Asma Jahangir imetayarishwa kwa malengo ya kisiasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ripoti iliyotayarishwa na ripota maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran ni ya kichochezi na haina hadhi wala uhalali.

Bahram Qassemi amesema kuwa, kimsingi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga kuteuliwa ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Iran na ripoti zake zinazotumwa katika Baraza Kuu la Haki za Binadamu ambazo zina sura ya kisiasa na si za kiadilifu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, ripoti zinazotayarishwa na ripota huyo zinatolewa kwa msingi wa azimio lisilokuwa la kiadilifu na kwa malengo ya kisiasa na matashi ya nchi kadhaa na kwamba ripoti hizo ni za kindumakuwili. Qassemi amesisitiza kuwa, Ripoti hizo zinadhoofisha nafasi ya Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuwafedhehesha wale wanaodai kutetea haki za binadamu na washirika wao ambao wana rekodi mbaya na nyeusi katika masuala ya haki za binadamu.

Asma Jahangir

Katika ripoti yake ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2017, Asma Jahangir ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran amekosoa tena utekelezaji wa sheria ya Kiislamu ya kisasi na kunyongwa walanguzi wa dawa za kulevya nchini Iran na kukariri madai ya kukiukwa haki za binadamu hapa nchini. 

Iran imekuwa ikitoa wito wa kukomeshwa tabia ya kutumiwa haki za binadamu kama wenzo wa kisiasa na kwa ajili ya kuzitwisha nchi nyingine fikra, utamaduni na mitazamo tofauti ya kisiasa.   

Tags