Takraibani asilimia 95 ya Wairani hawaiamini Marekani
Uchunguzi wa maoni umebaini kuwa asilimia 94.5 ya wananchi wote wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran hawaiamini Marekani na wanaitazama nchi hiyo kama adui.
Uchunguzi huo ulifanywa na shirika moja la uchunguzi wa maoni linalojulikana kama Kituo cha Afkar kati ya Oktoba 7-13 na kuwajumuisha watu wazima 863 kutoka miji mikuu ya mikoa yote 31 ya Iran.
Uchunguzi huo wa maoni uliochapishwa na Shirika la Habari la Tasnim, umebaini kuwa asilimia 60.6 ya Wairani hawaiamini Marekani hata kidogo huku asilimia 21.3 wakiwa wanasema Marekani haiaminiki na asilimia 12.5 wakisema kwa kiasi fulani hawaiamini Marekani.
Matokeo ya uchunguzi huo yanakuja mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye katika kampeni zake za uchaguzi alionyesha chuki za hali ya juu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wananchi wengi Iran wamechukizwa na uhasama wa Trump kuhusu mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na madola sita makubwa duniani na pia hatua ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo vipya kutokana na mfumo wake wa makombora ya kujihami.
Aidha katika hotuba yake hivi karibuni Trump alidai kuwa eti Iran ni nchi ya kigaidi na kutumia jina bandia la Ghuba ya Kiarabu kuashiria maji ambayo kihistoria yanajulikana kama Ghuba ya Uajemi. Uhasama huo wa Trump umezidi kuwakasirisha wananchi wa Iran.
Jana, kwa munasaba wa kutekwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran mwaka 1979, ubalozi ambao uligeuka na kuwa pango la ujasusi, kulifanyika maandamano dhidi ya Marekani kote Iran ambapo nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Trump' zilirindima.