Kiongozi asisitiza kupatiwa makazi walioathiriwa na tetemeko la ardhi magharibi mwa Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameshiriki katika kikao cha kuchunguza matatizo ya waliokumbwa na tetemeko la ardhi magharibi mwa Iran na kusema kipaumeble cha kwanza ni kuwajengea waathirika nyumba na kukarabati maeneo yaliyoharibiwa.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika mkoa wa Kermanshah uliokumbwa na zilzala hiyo, Ayatullah Khamenei ametoa wito kwa taasisi mbali mbali za kijeshi na zisizo za kijeshi zishirikiane katika kutekeleza kazi kwa kasi na kijihadi kwa lengo la kuwasaidia waathirika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masaibu na matatizo waliyonayo waliokumbwa na mtetemeko wa ardhi na kusema kabla ya tetemeko walikuwa wakiishi kwa utulivu pamoja kama familia na ghafla maisha yamebadilika katika msimu huu wa baridi na wanaishi katika mahema.
Ayatullah Khamenei amesema wakuu wa serikali wana jukumu zito katika kuwahudumia walioathirika na tetemeko huko Kermanshah huku akishukuru majeshi yote nchini kwa kuchukua hatua za kutoa huduma za awali na dharura punde baada ya tetemeko hilo. Amesema hatua za haraka zilizochukuliwa zilipelekea maisha ya watu wengi kuokolewa na kwamba kama si hatua hizo za awali za majeshi, watu wengi zaidi wangepoteza maisha.
Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha rishta lilitokea Jumapili usiku ya tarehe 12 Novemba magharibi mwa Iran. Watu 437 walifariki dunia na wengine zaidi ya 10,203 kujeruhiwa katika zilzala hiyo.