Velayati: Iran inajitolea muhanga kulinda usalama wa majirani zake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36721-velayati_iran_inajitolea_muhanga_kulinda_usalama_wa_majirani_zake
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye eneo hili ni wa kujivunia kwani ni ushawishi wa kirafiki na kwamba Tehran inajitolea muhanga kulinda usalama wa majirani zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2017 00:52 UTC
  • Velayati: Iran inajitolea muhanga kulinda usalama wa majirani zake

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye eneo hili ni wa kujivunia kwani ni ushawishi wa kirafiki na kwamba Tehran inajitolea muhanga kulinda usalama wa majirani zake.

Ali Akbar Velayati alisema hayo jana usiku katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na kanali ya pili ya televisheni ya Iran na kuongeza kuwa, lau kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingelizisaidia nchi za Iraq, Syria na Lebanon, hivi sasa Baghdad, Damascus na Beirut zingelikuwa zimetekwa na genge la kigaidi na la wakufurishaji la Daesh (ISIS).

Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amekumbushia pia uhakika wa kihistoria wa kupata ushindi mara zote Iran katika kujihami mbele ya maadui na kufafanua kwamba: Serikali halali za Syria na Iraq ziliiomba rasmi Iran kuzisaidia kupambana na Daesh na hayo yanatangazwa waziwazi na viongozi wa nchi hizo.

Shahid Hojaji, kijana wa Kiirani aliyejitolea kuwasaidia Waislamu wenzako nchini Syria na Iraq kupambana na magaidi wa Daesh. Aliuawa shahidi kwa kukatwa kichwa na magaidi hao

 

Amesema, katika hali ambayo nchi za Ulaya zinaungana na kuunda umoja wao kwa ajili ya kuwa na nguvu zaidi, katika upande wa pili zinaeneza fitna na ugomvi katika nchi za Mashariki ya Kati na za Kiislamu kwa lengo la kuzidhibiti.

Amesema Wamagharibi wanatumia fitna na hitilafu za kikaumu na kiitikadi kuzigombanisha nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa, kura ya maoni iliyoitishwa katika eneo la Kurdistan huko Iraq ni mfano wa wazi wa njama za Marekani na Wazayuni za kuzigawa vipande vipande nchi za Kiislamu kwa shabaha ya kuunda Israel nyingine pembeni mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq na Uturuki.