Ayatullah Kadhim Siddiqi: Kusambaratishwa ISIS kumeitia kiwewe Marekani na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36751-ayatullah_kadhim_siddiqi_kusambaratishwa_isis_kumeitia_kiwewe_marekani_na_israel
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amepongeza hatua ya kusambaratishwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) na kusisitiza kuwa, habari hizo zimechoma nyoyo za waungaji mkono wa magenge ya kigaidi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 24, 2017 13:02 UTC
  • Ayatullah Kadhim Siddiqi: Kusambaratishwa ISIS kumeitia kiwewe Marekani na Israel

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amepongeza hatua ya kusambaratishwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) na kusisitiza kuwa, habari hizo zimechoma nyoyo za waungaji mkono wa magenge ya kigaidi duniani.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi amesema kuangamizwa Daesh katika nchi za Iraq na Syria kumeudhalilisha sana utawala wa Kizayuni na dola la kiistikbari la Marekani.

Ayatullah Saddiqi amesema: "Ushindi wa hivi karibuni wa kung'olewa mizizi ya Daesh umetuma ujumbe mzito kwa wafadhili wa magenge ya kigaidi kote duniani, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel."

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amewafananisha waasisi na wafadhili wa ugaidi duniani kama mama mzazi aliyeshindwa na majukumu ya ulezi, na matokeo yake wamesababisha ukosefu wa usalama, machafuko na taharuki duniani.

Hujjatul Islam wal Muslimin Kadhim Siddiqi amesema njama za maadui za kuusambaratisha uliwengu wa Kiislamu katika vita vya siku 6, vita vya siku 33 na vita ya siku 51 zimegongwa mwamba na kuwatia kiwewe.

Vikosi vya Syria vikipeperusha bendera katika mji wa Bukamal

Ayatullah Saddiqi ameongeza kuwa: "Maadui wetu wanaoendesha kampeni za chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya Iran wataambulia patupu, kama walivyoshindwa maadui wa Mtume Muhammad SAW kumzuia kueneza Uislamu kote duniani."

Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi huu, komandi ya jeshi na vikosi vya ulinzi vya Syria ilitangaza rasmi kukombolea kikamilifu mji wa Deir ez-Zor kutoka mikononi mwa Daesh, na kuwatimua kabisa magaidi wakufurishaji wa ISIS waliouteka mji huo mwaka 2014.

Mji huo unapakana na mji wa al Qaima wa Iraq ambao nao tarehe 3 Novemba ulikombolewa na vikosi vya ulinzi vya Iraq, suala ambalo limerahisisha kukombolewa pia mji wa al-Bukamal wa Syria katika upande wa pili wa mpaka wa nchi hizo mbili.