Mar 14, 2018 02:45 UTC
  • Iran imebadilisha changamoto, vitisho kuwa fursa zisizo na kifani

Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema changamoto na vitisho vyote vya kigeni dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran vimebadilishwa na kuwa fursa zisizo na kifani.

Meja Jenerali Mohammad Ali Jaafari Kamanda wa IRGC  ameyasema hayo Jumanne katika kikao cha Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomteua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kamanda wa IRGC ameashiria njama za maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kumeshuhudiwa kushindwa kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS ambao ni wapinzani wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi za Iraq na Syria. Amesema huo ni ushindi mkubwa zaidi wa harakati ya mapambano ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Meja Jenerali Jaafari ameongeza kuwa: "Mwaka huu (wa 1396 Hijria Shamsia) umekuwa mwaka wa ushindi wa harakati ya mapambano au muqawama na mfano wa wazi ni kuangushwa ndege ya kivita ya F-16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo ilitunugliwa na jeshi la Syria katika hatua isiyo na kifani."

Kamanda wa IRGC  ameashiria kadhia ya Iraq na kusema: "Baada ya kuibuka kundi la ISIS, jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashd al Shabi lilijitokeza na kufuata nyayo za jeshi la kujitolea la wananchi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Basiji, ambalo liliundwa wakati wa vita vya kujihami kutakatifu. "Hu ni mfano wa kugeuza tishio kuwa fursa", amesisitiza Jaafari

Ayatullah Ahmad Jannati, Mwenyekiti wa Baraza Wanazuoni Wataalamu Wanaomteua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kamanda wa IRGC  ameongeza kuwa,  nchini Syria pia vikosi vya wapiganaji wa kujitoplea vya wananchi vimeundwa kukabiliana na ISIS na kwa msingi huo Iraq na Syria zimebadilisha njama za maadui kuwa fursa.

Meja Jenerali Jaafari amekumbusha kuwa uwezo mkubwa wa kujihami wa Iran hasa makombora ni miongoni mwa sababu za ushindi wa harakati ya muqawama na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya maadui.

Kikao cha Nne cha Baraza Wanazuoni Wataalamu Wanaomteua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilianza jana Jumanne kwa hotuba ya Mwenyekiti wa baraza hilo Ayatullah Ahmad Jannati.

Tags