Rouhani: Iran na Russia zitaendelea kushirikiana hadi usalama urejee Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42900-rouhani_iran_na_russia_zitaendelea_kushirikiana_hadi_usalama_urejee_syria
Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zitaendelea kuwa na uhusiano wa kistratajia na ushirikiano wa karibu hadi usalama, utulivu na uthabiti urejee kikamilifu nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 09, 2018 23:19 UTC
  • Rouhani: Iran na Russia zitaendelea kushirikiana hadi usalama urejee Syria

Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zitaendelea kuwa na uhusiano wa kistratajia na ushirikiano wa karibu hadi usalama, utulivu na uthabiti urejee kikamilifu nchini Syria.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake hapa Tehran na Mwenyekiti wa Bunge la Chini la Russia (Duma),  Vyacheslav Volodin na kubainisha kuwa, "Uhusiano wa karibu na ushirikiano kati ya Iran na Russia umekuwa na matokeo mazuri katika mchakato wa kuhakikisha kuwa, sio Syria tu bali nchi zote za eneo la Mashariki ya Kati zinakuwa na usalama, amani na uthabiti; na ushirikiano huu utaendelea hadi tuhakikishe kuwa usalama umerejea kikamilifu nchini Syria."

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Bunge la Chini la Russia (Duma),  Vyacheslav Volodin amesema kuwa, Tehran na Moscow zinakabiliwa na changamoto za kieneo na kimataifa zenye kufanana na kwa msingi huo, nchi yake itaendelea kushirikiana na Iran ili kwa pamoja ziandae ramani ya njia ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran na mwenzake Vladimiri Putin wa Russia

Aprili 4, Marais wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki walikutana mjini Ankara kwa uenyeji wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na kujadiliana mgogoro wa Syria.

Saudi Arabia, Marekani, Israel na madola mengine adui yamelibebesha taifa la Syria mzigo wa vita na ukosefu wa amani kupitia magenge ya kigaidi hasa Daesh kwa miaka saba sasa, kwa lengo la kuivunja nguvu kambi ya muqawama iliyosimama imara kupambana na dola pandikizi la Israel lakini njama hizo zimefeli.