Shamkhani: Marekani haina uthubutu wa kuishambulia kijeshi Iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran sambamba na kubainisha kwamba vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran ya Kiislamu vimefeli amesisitiza kwamba, nchi hiyo ya Magharibi haina uthubutu wa kuishambulia kijeshi nchi hii.
Admeri Ali Shamkhani aliyasema hayo Jumatano ya jana kupitia mahojiano na televisheni ya al-Jazirah ya Qatar hasa kuhusiana na shambulizi la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni nchini Syria na jibu kali lililotolewa na jeshi la Syria na kusema, utawala wa Israel umepata ujumbe wa wazi kabisa nao ni kwamba, kila hujuma itakayoifanya nchini Syria, basi itakuwa na jibu kali la moja kwa moja na bila shaka yoyote Damascus itakabiliana na hujuma hizo.
Kadhalika Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran sambamba na kubainisha kwamba makombora ya Iran ni kadhia ambayo haikubali kujadiliwa ameongeza kuwa, Iran si tu kwamba haitojadiliana na nchi yoyote kuhusiana na makombora yake, bali ni kwamba Tehran itaendelea kuimarisha uwezo wake wa makombora hayo. Aidha ameashiria uungaji mkono wa Iran kwa makundi ya muqawama katika eneo la magharibi mwa Asia na kusisitiza kwamba, Iran itaendeleza uungaji mkono wake huo kwa harakati zote za muqawama wa Palestina kuanzia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS, Harakati ya Jihadul-Islami na Harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon na muqawama wote katika eneo.
Aidha Ali Shamkhani amezungumzia hali ya sasa nchini Yemen na ukwamishaji wa Saudia katika kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu na kusema, Harakati ya Wananchi ya Answarullah ya nchi hiyo ilikubali pendekezo la Umoja wa Ulaya la kufanyika mazungumzo kipindi hiki lakini Saudia imekataa pendekezo hilo.