Qassemi: Marekani inatumia vibaya dini kuzusha ugomvi katika baadhi ya mataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu ripoti iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu uhuru wa kidini duniani na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiona ripoti hiyo kuwa haikuzingatia ukweli wa mambo, haina mashiko wala msingi wowote bali imetolewa kwa malengo ya kiuadui na kwa shabaha ya kutumia vibaya dini kwa malengo ya kisiasa.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imedai katika ripoti yake ya uhuru wa kidini ya mwaka 2017 ambayo imetolewa Jumanne wiki hii kuwa eti hakuna uhuru wa kidini nchini Iran.
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo Alkhamisi amejibu ripoti hiyo kwa kusema, Marekani inapaswa kuchunga maadili ya kusema vitu ilivyo na welewa na elimu navyo na iwapo itajiepusha kutoa tafsiri za kubuni na zisizo na mashiko kuhusu itidaki za kidini itaepusha kutokea mivutano ya kidini duniani.
Vile vile amesema, Marekani inapaswa kuheshimu njia za mazungumzo na kuheshimiwa itikadi za dini nyingine na sio kusema mambo isiyo na elimu nayo.
Amesema, lengo la Marekani ni kutumia vibaya kisiasa muundo wa kijamii wa watu wa dini tofauti katika mataifa mbalimbali duniani na inashindwa hata kufanya tathmini ya kina ya kuzingatia uhalisia wa mambo wa nchi za jamii hizo.
Aidha amesema wananchi wa Iran wana ustaarabu na utamaduni tajiri wa maelfu ya miaka na kwamba jamii za watu wote zinaishi kiudugu nchini Iran bila ya kujali makabila na itikadi zao za kidini.
Aidha amesema,m baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wafuasi wa dini na madhehebu zote wanaendelea kuendesha shughuli zao za kidini kwa uhuru kamili nchini Iran kwa mujibu wa Katiba na sheria na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina wasiwasi wowote kuhusu uhuru huo mkubwa wa kidini uliopo nchini.