Iran haifanyi mazungumzo yoyote na utawala wa Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema maadamu Marekani haitumii lugha ya heshima na haiachi kutumia vitisho wakati wa kuzungumza na taifa kongwe na lenye ustaarabu la Iran, basi hakuna uwezekano wowote wa kuwepo mazungumzo katika uga wowote baina ya Iran na Marekani.
Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa tamko hilo leo Ijumaa katika kujibu matamshi ya Rais wa Marekani kuhusu kuiwekea Iran vikwazo ambavyo havina kifani na wakati huo huo kusema eti ana matumaini kuhusu kufikiwa mapatano kamilili na Iran.
Qassem amesema: "Katika kipindi chote cha historia iliyojaa fahari, Wairani wameonyesha kuwa kamwe vitisho haviwezi kubadili fikra, amali na mwenendo wao uliojaa hekima."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni mfano wa wazi wa namna Marekani inavyokiuka mapatano na sheria za kimataifa.
Aidha Qassemi amesema taifa la Iran, kwa kutegemea uwezo na umahiri, halijawahi kusalimu amri mbele ya vikwazo vya tawala mbali mbali za Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: "Serikali ya Marekani, kwa kutumia ugaidi wa kiuchumi, haiwezi kuvuruga irada ya taifa la Iran ambalo limeazimua kulinda uhuru wake sambamba na kupambana na ugaidi ili kuleta uthabiti, usalama na ustawi wa kiuchumi katika eneo.
Qassemi aidha amesema badala ya Rais Donald Trump kutafakari kuhusu eti mapatano kamili na Iran, kwanza asitishe sera zake za vikwazo, mashinikizo na kukiuka mikataba na nchi zingine duniani.