Qassemi: EU ichukue uamuzi haraka kuhusu namna ya kuendeleza JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45720-qassemi_eu_ichukue_uamuzi_haraka_kuhusu_namna_ya_kuendeleza_jcpoa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameutaka Umoja wa Ulaya uchukue uamuzi haraka kuhusu namna makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yataweza kuendelezwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2018 10:31 UTC
  • Qassemi: EU ichukue uamuzi haraka kuhusu namna ya kuendeleza JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameutaka Umoja wa Ulaya uchukue uamuzi haraka kuhusu namna makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yataweza kuendelezwa.

Bahram Qassemi ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi wakati akizungumzia kuendelezwa makubaliano ya JCPOA. Amefafanua kuwa: Kutokana na Marekani kujitoa kinyume cha sheria katika makubaliano haya ya kimataifa, inapasa Umoja wa Ulaya utoe hakikisho kuhusu namna manufaa na maslahi ya Iran yatadhaminiwa na kukidhiwa katika JCPOA.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: Umoja wa Ulaya ni majimui kubwa na yenye mfumo maalumu wa urasimu, lakini kama EU inataka Iran ibakie kwenye JCPOA inapaswa kuchukua maamuzi haraka na yenye uwazi kabisa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (wa pili kushoto) alipokutana kwa mashauriano na maafisa waandamizi wa nchi za Ulaya kujadili hatima ya JCPOA

Kuhusu wasiwasi wa nchi za Ulaya juu ya mpango wa makombora na masuala ya kieneo ya Iran, Qassemi amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka eneo liwe na amani, usalama na uthabiti; suala ambalo litapatikana kwa maafikiano na ushiriki wa nchi zote za eneo hili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia pia kikao cha Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un, kitakachofanyika kesho nchini Singapore na kueleza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha hatua ya kurejesha amani na utulivu katika Peninsula ya Korea, lakini Korea Kaskazini inapaswa kuwa macho na makini katika uhusiano wake na Marekani kwa sababu Washington imeonyesha kuwa si ya kuaminika sana, na hilo linathibitishwa na matukio tofauti yaliyojiri duniani.../