Naibu Waziri wa Ulinzi: Iran itaimarisha uwezo wake wa makombora
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa na uwezo wa makombora ya balistiki na cruise na kumiliki ndege za kivita za kizazi kipya pamoja na manowari na nyambizi za kisasa zenye uwezo wa kuenda masafa ya mbali ni kati ya mipango inayofuatiliwa na Wizara ya Ulinzi ya Iran.
Brigedia Mohammad Ahadi ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran alipokutana na wambata wa kijeshi wanaowakilisha nchi zao hapa Iran na kuongeza kuwa, vikwazo haviwezi kusitisha mchakato wa kuimarisha uwezo wa kujihami nchini Iran. Amebainisha kuwa, ili kuimarisha uwezo wa kujihami kunahitajika miundo msingi muhimu.
Brigedia Ahadi amepongeza jitihada za wambata wa kijeshi katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi zao na Iran. Amesema mtazamo wa Iran kuhusu udiplomasia wa kujihami umejengeka katika msingi wa kuwa na uhusiano na wote isipokuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu. Amesema katika udiplomasia wake wa kujihami, Iran inalenga kusaidia upatikanaji wa amani na usalama katika eneo hili na duniani kiujumla pamoja na kuzuia migogoro.
Aidha ameashiria nafasi muhimu ya Iran katika vita dhidi ya ugaidi na kusema, iwapo Iran na waitifaki wake Syria na Iraq, hawangechukua hatua za kuzuia kundi la kigaidi la ISIS leo ramani ya kijiografia katika eneo ingebadilika na dunia ingelikumbwa na changamoto kubwa na hatari.
Brigedia Ahadi amesema mgogoro wa Yemen umepelekea kuibuka maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika karne hii. Amebainisha kuwa jeshi vamizi la Saudia linapata silaha kutoka nchi kadhaa za Magharibi na kwamba inatia aibu kuona namna jamii ya kimataifa ilivyonyamazia kimya hujuma dhidi ya Yemen.
Katika kikao hicho wambata wa kijeshi wa nchi za kigeni walitembelea maonyesho ya mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran.