Rais Rouhani: Maadui hawawezi kuizuia Iran katika mkondo wa ustawi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui hawana uwezo wa kulizuia taifa la Iran katika mkondo wake wa ustawi.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika mji wa Asalouyeh kusini mwa Iran wakati akizindua miradi kadhaa mikubwa ya viwanda vya petrokemikali. Rais Rouhani amesema wafanyakazi wa sekta ya mafuta leo wamechukua hatua kubwa kuiletea Iran heshima na kubuni nafasi za ajira na kuongeza kuwa: "Kufunguliwa miradi mitatu mikubwa ya petrokemikali katika siku moja ni jambo linalothibitisha wazi kuwa tutavuka matatizo na maadui hawataweza kuzuia mkondo wa ustawi wa taifa la Iran."
Rais Rouhani amesema kuwa adui atafanikiwa tu wakati ataweza kuondoa matumaini na kusitisha harakati ya taifa. Ameongeza kuwa, maadui wanawaletea wananchi matatizo lakini ni muhali waweze kudhibiti Iran na Wairani na hawatafikia ndoto yao ya kuona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikirejea katika zama za kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Miradi ya petrokemikali ambayo Rais Rouhani ameizindua leo huko Asalouyeh ina thamani ya dola bilioni 1.85 na inajumuisha viwanda va methanoli, urea na ammonia.