Jeshi la Iran liko tayari kujibu tishio lolote la usalama dhidi yake
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, pamoja na kwamba Iran haikabiliwi na hatari au tishio la aina yoyote la usalama, lakini imejiandaa kutoa jibu kali kwa chokohoko zozote za maadui.
Brigedia Jenerali Kioumars Haydari ameyasema hayo leo Jumapili akiwa mkoani Hamedān, magharibi mwa Iran na kuwahakikishia wananchi kwamba nchiyao haiko katika ncha ya kuingia vitani.
Amebainisha kuwa, "Hata kama Iran haikabiliwi na tishio lolote la usalama lakini jambo hilo halina maana kuwa jeshi la taifa limeweka pembeni sera yake ya kuwa tayari kukabiliana na uchokozi wa maadui wakati wote, kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara zote Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei."
Vile vile Brigedia Jenerali Kioumars Haydari amepongeza namna vikosi vya ulinzi vya Iran vilivyo tayari wakati wote kulinda usalama wa nchi na kusisitiza kuwa, uwezo wa kujihami wa taifa hili umepiga hatua kubwa kiasi kwamba, wanaotafuta uadui na Iran kwa sasa wamegeukia uadui usiokuwa wa kijeshi.
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, uwezo mkubwa wa jeshi la Iran unaweza kuzima chokochoko za maadui katika muda mfupi mno.