Sayyid Araqchi: Kuzungumza na Iran kwa lugha ya vitisho hakuna faida
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48453-sayyid_araqchi_kuzungumza_na_iran_kwa_lugha_ya_vitisho_hakuna_faida
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameihutubu serikali ya Marekani akiiambia kwamba, kuzungumza na taifa la Iran kwa lugha ya vitisho katu hakuwezi kuwa na faida si sasa hivi tu bali hata katika siku za usoni.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Sep 28, 2018 23:14 UTC
  • Sayyid Araqchi: Kuzungumza na Iran kwa lugha ya vitisho hakuna faida

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameihutubu serikali ya Marekani akiiambia kwamba, kuzungumza na taifa la Iran kwa lugha ya vitisho katu hakuwezi kuwa na faida si sasa hivi tu bali hata katika siku za usoni.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya TRT ambapo sambamba na kuashiria njama za Rais Donald Trump wa Marekani za kulzusha anga hasi dhidi ya Iran amebainisha kwamba, hatua hizo za Trump hazijaungwa mkono na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema wazi kuwa, misamiati michafu na ya kiuadui inayotumiwa na Trump dhidi ya Iran ni jambo lililozoeleka, lakini Tehran haitamjibu ila yule anayezungumza nayo kwa lugha ya heshima.

Donald Trump, rais wa Marekani mwenye kupenda kutumia lugha chafu dhidi ya Iran

Akijibu swali la mtangazaji wa Kanali ya Televisheni ya TRT kwamba, kutengwa Marekani na kuungwa mkono Iran na mataifa mengine baada ya kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kinyume na matarajio ya Trump, Sayyid Abbas Araqchi amesema, JCPOA ni makubaliano ya kimataifa yanayoihusu jamii yote ya kimataifa ambapo hatua ya Washington ya kujitoa katika makubaliano hayo imekiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akijibu swali kwamba, je vita vya maneno vya Iran na Marekani vitaishia katika vita vya kijeshi, Abbas Araqchi amesema, Iran imejiandaa kikamilifu hata katika mazingira mabaya kabisa na sidhani kama Marekani itakuwa na ufahamu finyu kiasi cha kuamua kuanzisha vita na Iran.