Amano ajibu madai ya Netanyahu dhidi ya Iran, asema IAEA inajitegemea
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amekanusha madai yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa, wakala huo unafanya kazi kwa kujitegemea na hautilii maanani madai yanayotolewa na upande mwingine.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo kujibu madai yaliyotolewa na Benjamin Netanyahu dhidi ya Iran, Yukia Amano amesisitiza kuwa, madai yanayotolewa na upande mwingine yanapaswa kuchunguzwa kwa makini na kutathiminiwa na kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia unafanya kazi kwa kujitegemea. Amesisitiza kuwa shughuli za wakala huo nchini Iran zinafanyika kwa mujibu wa makubaliano kamili ya CSA.
Mkurugenzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia amesema kuwa shughuli zote za usimamizi wa miradi ya nishati ya nyuklia nchini Iran zinaendelea katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba wakala huo unaruhusiwa kukagua maeneo yote.
Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel, Benjamin Netanyahu tarehe 27 Septemba alisimama katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York akiwa ameshikilia picha na kudai kwamba, Iran ina ghala katika mji wa Tehran ambalo lina zana za nyuklia ambazo haijaziripoti kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.