Papa Francis: Iran ni nchi yenye utamaduni tajiri na ustaarabu mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49184-papa_francis_iran_ni_nchi_yenye_utamaduni_tajiri_na_ustaarabu_mkubwa
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema, sifa kubwa maalumu ya taifa la Iran ni kuwa kwake na utamaduni tajiri wa kiutu ambao unaweza kutumiwa kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu wa zama hizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2018 12:52 UTC
  • Papa Francis: Iran ni nchi yenye utamaduni tajiri na ustaarabu mkubwa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema, sifa kubwa maalumu ya taifa la Iran ni kuwa kwake na utamaduni tajiri wa kiutu ambao unaweza kutumiwa kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu wa zama hizi.

Papa Francis ameyasema hayo katika mazungumzo na Hujjatul-Islam Sayyid Taha Hashemi, balozi mpya wa Iran mjini Vatican na akaongeza kuwa, anakaribisha mazungumzo anayofanya kila mara na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ameyataja kama kielelezo cha mazungumzo baina ya dini mbalimbali.

Baada ya kukabidhi nakala ya hati zake za utambulisho kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Sayyid Hashemi, balozi mpya wa Iran mjini Vatican amesema, siasa haribifu na zenye madhara za baadhi ya nchi ikiwemo Marekani ndio chanzo cha masaibu na matatizo mengi yanayoikabili jamii ya mwanadamu hivi sasa.

Amefafanua kuwa, sera za kujichukulia hatua za upande mmoja za Marekani katika uga wa kimataifa ikiwemo kujitoa kwenye mikataba ya kimataifa kama mkataba wa kupiga marufuku makombora ya nyuklia ya masafa ya kati, mkataba wa tabianchi wa Paris na muhimu zaidi makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zimevuruga amani ya dunia na eneo la Mashariki ya Kati na kuwatumbukiza walimwengu kwenye enzi mpya za Vita Baridi.

Rais Hassan Rouhani wa Iran (wa tatu kushoto) alipotembelea Vatican na kuonana na Papa Francis

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vatican amesisitizia ulazima wa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali pamoja na fikra za waliowengi duniani kulaani sera na uchukuaji hatua na maamuzi ya upande mmoja.

Aidha katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican Petro Parolin, Sayyid Taha Hashemi ameashiria sera hatari za Marekani baada ya kuingia madarakani rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump na kueleza kwamba: Siasa haribifu za serikali ya sasa ya Marekani zimesababisha kuenea zaidi ukosefu wa amani na kuzidi kuvuruga uthabiti hususan katika eneo la Mashariki ya Kati na kuwafanya wahanga watu wasio na hatia, kutishia usalama wa jamii za wachache na kusababisha wimbi jipya la wahajiri.

Kwa upande wake, Petro Parolin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican amesema, anatiwa wasiwasi na mielekeo ya kujichukulia hatua za upande mmoja ya baadhi ya nchi ikiwemo Marekani na akasisitiza kwamba: Haipasi wananchi wa mataifa ya dunia wawe kwenye mashinikizo kutokana na siasa za baadhi ya nchi.../