Iran yazima hujuma ya Israel katika mitandao ya mawasiliano
Iran imefanikiwa kuzima wimbi la mashambulizi kupitia intaneti (cyber-attack) ambayo yalikuwa yametekelezwa na utawala haramu wa Israel kwa lengo la kuvuruga mitandao ya mawasiliano nchini.
Katika taarifa kupitia mtandao wa Twitter siku ya Jumatatu, Hamid Fatahi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Iran amesema uhasama huo utafuatiliwa kupitia vyombo vya sheria katika uga wa kimataifa.
Amesema wataalamu wa Iran wamezima hujuma hizo za mitandaoni kikamilifu. Naye Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Iran Mohammad-Javad Azari Jahromi amesema utawala wa Kizayuni wa Israel una faili chafu la kutumia silaha ya mitandao ya intaneti dhidi ya Iran na mfano wa hilo ni shambulizi la miaka ya nyuma kupitia kirusi cha Stuxnet.

Amesema mara hii utawala wa Kizayuni ulikuwa umelenga kuvuruga miundo msingi ya mawasiliano nchini Iran. Amesema utawala wa Kizayuni umeambulia patupu kutokana na kuwa macho wataalamu wa Iran na amesisitiza kuwa Iran itawasilisha mashtaka kimataifa kufuatua uhasama huo.
Mwaka 2011 utawala wa Kizayuni wa Israel ulitekeleza shambulizi la kupitia mitandao ya intaneti dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran kwa kutumia kirusi cha Stuxnet.